TUNDU Lissu, Mbunge wa Singida Mashariki amesema, ‘namtaka dikteta uchwara mahakamani,’.
Lissu
ambaye ni Mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni amesema hayo leo
muda mfupi baada ya kutoka kusikiliza shauri lake katika Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam la kudaiwa kutoa kauli ya
uchochezi.
“Mimi na jopo langu la mawakili tunamtaka niliyemuita diktekta uchwara aje mahakamani kuthibitisha udikitekta uchwara wake,” amesema Lissu.
Lissu
amefunguliwa shitaka la uchochezi katika mahakama hiyo, kesi yake
inasikilizwa na Hakimu Yohona Yongolo ambapo kwa upande wa mashitaka,
unawakilishwa na Benard Kongolo, wakili wa serikali mkuu.
Lissu
alijisalimisha jana 5 asubuhi katika kituo hicho cha polisi ambapo
alizuiliwa kupewa dhama na kulala hadi alipofikishwa mahakamani leo.
Wafuasi
na viongozi mbalimbali wa Chadema walifika mahakamani hapo akiwemo
Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa chama hicho taifa; Salum Mwalim, Kaimu
Katibu Mkuu Zanzibar na Benson Kigaila, Mkuu wa Operesheni wa chama
hicho.
Wakili
Kongolo amedai kuwa, Lissu alitenda kosa hilo tarehe 28 Juni mwaka huu
katika eneo la Mahakama ya Kisutu jijini Dar es Salaam kwa kuzungumza;
“Mamlaka
ya Serikali mbovu ni ya kidiktekta uchwara inahitaji kupingwa na kila
Mtanzania kwa nguvu zote, huyu dikitekta uchwara lazima apingwe kila
sehemu kama uongozi utafanywa na utawala wa kijinga nchi inaingia ndani
ya giza nene.’’
Hata
hivyo, Lissu amekana shitaka hilo, amedhaminiwa na wadhamini wawili
waliosaini hati ya Sh.2 milioni kila mmoja na masharti ya kutosafiri nje
ya nchi na kwamba, upelelezi wa kesi hiyo umekamilika. Kesi hiyo
itatajwa kwa kusikilizwa tarehe 2 Agosti mwaka huu.
Upande
wa utetezi uliwakilishwa na mawakli 11 miongoni mwao ni Michael Ngolo,
Peter Kibatala, John Mallya, Hekima Mwasibu, Omari Msemo, Jeremia
Mutasebya na Juma Nasoro.
Nje ya Mahakama
Alipotoka
nje ya mahakama Lissu alizungumza na wafuasi wa Chadema waliofurika
katika viwanja hivyo pamoja na waandishi wa habari ambapo amesema,
“nilijua kwamba wenye busara watanyamaza baada ya mimi kutoa kauli ile
juzi mahakamani hapa."
Hata
hivyo, Lissu amesema kuwa, katika kituo alicholazwa ameshuhudia watu
wakiteseka kutokana na kutopelekwa mahakamani kwa muda wa wiki mbili
hadi mwezi mmoja na kuwa, hupewa mateso makali mpaka kusababisha wengine
kuvunjwa miguu.
Mbowe
amewaambia waandishi wa habari kuwa, uonevu wa utawala wa sasa
unafanywa bungeni na nje ya bunge na kwamba, hawatakata tamaa ya
kupigania haki.
Wakati
huo huo Jeshi la Polisi limewatia mbaroni wafuasi wanne wa Chadema
walikuwa wamebeba mabango yenye maneno ‘Dikitekta Uchwara nenda
Burundi,’ Polisi ‘Uchwara acheni kutumika’ na ‘Lisuu Tanzania
inakuhitaji.’

