KIONGOZI wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, amesema Chama Cha Mapinduzi (CCM) hata kipate malaika hakiwezi kubadilika, hivyo dawa pekee ni kukiondoa jumla madarakani.
Akizungumza
juzi wakati wa mkutano wa kampeni uliofanyika katika kituo cha basi
Tabata Segerea, Zitto alisema matatizo mengi ya nchi yamesababishwa na
sera mbovu za CCM ambazo baadhi ya wagombea wake ndio waliokuwa
wakizitunga, kuzitetea na kuzitekeleza.
“Kuna
ambao wamekuwa watawala tangu tupate uhuru na bado wanataka waendelee
kutawala, ukiwauliza wanasema tupeni tena kipindi kingine.
“Sisi
tunataka wote waondoke, tunataka tuweke mwanzo mpya katika nchi hii
ndio maana hata ilani yetu imejikita kutatua changamoto mbalimbali
zinazotukabili,” alisema Kabwe.
Zitto
aliyewasili viwanjani hapo saa 10:14 jioni na kuanza kuhutubia saa
11:13 jioni, alisema taifa linakabiliwa na changamoto kuu nne ambazo ni
umaskini, huduma mbovu za jamii, kukosekana kwa umoja wa kitaifa na
ufisadi.
“Leo
hii tumekua na uchumi ambao hauzalishi ajira na kusababisha vijana
wengi wanaomaliza masomo yao kuhangaika kutafuta kazi. Ni kwanini uchumi
ambao unakua kwa kasi hauzalishi ajira,?” alihoji Kabwe.
Alisema
hivi sasa nchi imekuwa na matabaka kwenye huduma za jamii kama vile
elimu na afya na kusababisha Taifa kuwa la masikini na matajiri.
“Leo
hii watoto wa masikini na matajiri hawakutani, wa matajiri wanasoma
shule zao halikadhalika na wa masikini…matajiri wanafundishwa elimu bora
wanaandaliwa kuja kuwatawala masikini.
“Rushwa
kubwa ndio inalitafuna taifa hili, mwaka jana zilitengwa Sh bilioni 546
kwa ajili ya kununulia madawa muhimu lakini ni Sh bilioni 36 tu ndizo
zimetolewa, kuna wajanja wachache wamezifanyia ufisadi zile fedha,” alisema.
Kiongozi
huyo wa ACT, alisema wamejipanga vizuri na wamesimamisha wagombea
ubunge 219 nchi nzima hivyo akawataka Watanzania kuwapima kulingana na
uwezo wao kisha kufanya uamuzi.
Awali
mgombea ubunge katika Jimbo la Segerea, Mohamed Mwikongi, alisema
akifanikiwa kushinda kiti hicho ataanzisha mfuko wa maendeleo wa Segerea
na kuwahamasisha wananchi wajiunge katika vikundi ili wapate mikopo.
“Nitaangalia
upya mfumo wa wazazi kuchangia gharama za elimu katika shule za umma na
kuzipunguza ili ziendane na hali halisi ya utendaji,” alisema Mwikongi.
Naye
mjumbe wa chama hicho, Terry Gbemundu, alisema Watanzania wengi
wameaminishwa kuwa ni masikini lakini hakuna umasikini wowote nchini.
“Tunaaminishwa hivyo ili tuibiwe tuzidi kukandamizwa, akili zimedumazwa lakini sasa uamuzi mnao kwenye sanduku la kura.
“Atakayechagua kijani (akimaanisha CCM) ambayo imetawala kwa miaka 54 bila mafanikio sijui itabidi tukapimwe akili,” alisema Gbemundu.
0 comments:
Chapisha Maoni