test

Jumamosi, 29 Agosti 2015

Mwakyembe Amshambulia LOWASSA Kuhusu Sakata la Richmond...........Mwigulu Nchemba naye Adai Lowassa Ni Mpiga Dili Tangu Kijana...




Aliyekuwa mwenyekiti wakamati teule ya bunge ya kuchunguza kashfa ya mkataba tata wa Richmond iliyomuondoa madarakani aliyekuwa waziri mkuu Mh Edward Lowassa, Mh Harrsion Mwakyembe amewahakikishia watanzania kuwa walijiridhisha pasipo shaka kuhusika kwa Edward Lowassa katika sakata la Richmond na kwamba hawakumsingizia kama anavyojitetea hivi sasa.
 
Mwakyembe aliyasema hayo mbele ya maelfu waliojitokeza katika mkutano wa hadhara wa mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli katika viwanja vya Luandanzovwe jijini Mbeya, jana.

Akizungumzia madai ya kwa nini baadhi ya wahusika hawakupelekwa mahakamani kama kuna ushahidi, mhadhiri huyo wa sheria alisema kosa la jinai, halina ukomo na wakati wowote linaweza kufunguliwa mashitaka, huku akiapa kuwa anaweza kumfungulia mtu mashitaka hata kesho.

Alionya viongozi na makada wa Chadema na vyama vinavyowaunga mkono katika umoja wa Ukawa wanaozindua kampeni zao leo jijini Dar es Salaam, kwamba wasithubutu kujibu hoja zake.

Dk Mwakyembe alisema ikilazimika kusema ukweli, ataweka hadharani uchafu wote uliofanyika, ambao alisema bungeni kuwa asingeuanika na kuifanya Richmond hoja ya kila siku mpaka Watanzania waelewe kilichofanyika.

“Tunao ushahidi. Hawa walitakiwa kuwa jela badala ya kuimba nyimbo za ajabu,” alisema Dk Mwakyembe katika mkutano huo uliorushwa moja kwa moja nchi nzima na kuongeza kuwa Dk Magufuli akiingia madarakani, anakwenda kuanzisha Mahakama ya Ufisadi.

Alisema yeye na wenzake walipewa kazi ya Bunge kuchunguza ilikuwaje viongozi waandamizi wakaamua kuipa kampuni hewa zabuni ya mabilioni ya fedha, ambayo imesababisha mpaka leo kuna shida ya umeme nchini.

Dk Mwakyembe alikumbusha kuwa walikwenda mpaka Marekani kuchunguza uwepo wa kampuni hiyo iliyodaiwa kutoka katika nchi hiyo, na kukutana na kampuni ya kuchapisha kadi za harusi.

Kwa mujibu wa Dk Mwakyembe, baada ya kubaini ubadhirifu huo, aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, alishinikizwa kujiuzulu na kumaliza suala hilo na hivyo hatua ya kiongozi huyo kutaka kwenda Ikulu, wazalendo hawawezi kuikubali.

“Hatutaruhusu watumie demokrasia kuingia Ikulu na hiyo ndiyo shida ya kuazima wagombea,” alisema Dk Mwakyembe akimaanisha kuwa chama cha Chadema, kimeazima mgombea bila kumfahamu.
 
 Dk Mwakyembe alisema suala hilo lilishafungwa bungeni, lakini anashangaa kusikia linarejeshwa kinyemela.

Mwigulu
Naye Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi, Mwigulu Nchemba, alisema mgombea wa Ukawa, Lowassa, tangu akiwa kijana alikuwa ‘mpiga-dili’.

Kwa mujibu wa Mwigulu, Rais Kikwete alipoingia madarakani, alidhani kuwa Lowassa alikuwa ameonewa, akamteua kuwa Waziri Mkuu, lakini kabla ya kumaliza miaka miwili, akaendeleza tabia yake ya ‘kupigadili’.

Mwigulu alionya kuwa, Watanzania wakimpeleka ‘mpiga-dili’ Ikulu, shida yake na wenzake si changamoto za watu wa Mbeya wapate maji, huduma bora za afya na nyingine bora za umma, bali kurejesha fedha walizotumia wakati wa kutafuta urais.

“Mkimpeleka mpiga dili Ikulu, ‘wapiga-dili’ wenzake hawatalipa kodi, mtalipa nyie wanyonge ili wale ‘wapigadili’ warejeshe fedha zao,” alisema na kufafanua sababu za vyama vya Chadema, CUF, NCCRMageuzi na NLD kuungana pamoja katika Ukawa. 
 
Kwa mujibu wa Mwigulu, kilichowaunganisha ni maslahi ya aina mbili; moja aliyetoa fedha kwa ajili ya kwenda Ikulu, ambaye anatafuta nafasi hiyo ili arejeshe madeni yake na wengine ni waliouza vyama ambao ‘wameshakunja’ chao.

“Nawaambia mwisho wa mbwembwe na maigizo, ni Oktoba 25 na baada ya hapo ni kazi tu,” alisema Mwigulu na kuhoji iweje Lowassa apande daladala leo, ambalo hakulipanda miaka 40 iliyopita?
 
 Mwigulu alisema Watanzania wana siku 60 za kujadili hatima ya taifa lao na katika hilo, hakuna namna zaidi ya kuelezana ukweli mtupu.

Install Application ya JUNGUKUULEO Uweze Pata Habari Kirahisi Zaidi

xxxxxxxxxxxxx

0 comments:

Chapisha Maoni