Mwenyekiti
wa Chadema, Freeman Mbowe jana aliugua ghafla akiwa katika maandamano
ya kumsindikiza mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho, Edward Lowassa
baada ya kuchukua fomu za kugombea urais katika Tume ya Taifa Uchaguzi
(NEC).
Mbowe
alishiriki katika maandamano yaliyoanzia Makao Makuu ya CUF yaliyopo
Buguruni wilayani Ilala kuelekea NEC na baada ya Lowassa kuchukua fomu,
mwenyekiti huyo aliendelea na msafara kwenda Kinondoni yalipo makao
makuu ya Chadema.
Wakiwa
njiani Mbowe na Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu walikuwa
wamechomoza kwenye gari wakiwapungia wananchi waliojitokeza kwenye
maandamano hayo.
Hali
ya Mbowe ilibadilika ghafla na aliamua kushuka juu ya gari na kukaa
katika kiti, ndipo Lissu na watu waliokuwamo kwenye gari hilo wakaanza
kumpatia huduma ya kwanza kwa kumfungua vifungo vya shati lake katika
eneo la Kinondoni kwa Manyanya.
Wakati
hali ya Mbowe ilipoanza kubadilika msafara wa Lowassa ulikuwa ukielekea
katika Uwanja wa Biafra, Kinondoni na magari yalikuwa yakitembea mwendo
mdogo kutokana na maelfu ya watu waliokuwa wakiandamana.
Wakati
maandamano hayo yakiendelea, gari lililombeba Mbowe likiwa na walinzi
wa Chadema walioning’inia milangoni, lilichomoka katika msafara huo
ambao ulikuwa umeingia Barabara ya Kawawa na lilikunja kona katika
barabara ya kuelekea Mahakama ya Kinondoni kwa ajili ya kumwahisha
hospitali na taarifa zilizopatikana baadaye zilieleza kuwa lilielekea
katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).
Akizungumzia hali hiyo, Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki, alisema kuwa Mbowe yuko salama na anaendelea vizuri.
“Ni uchovu, uchovu, uchovu tu but he is out of danger (hayuko katika hali ya hatari),” alisema Lissu.
Ofisa
Uhusiano wa MNH, Aminiel Aligaesha alisema walimpokea Mbowe saa 11
jioni na alikuwa anaendelea na matibabu katika hospitali hiyo, hata
hivyo hakutaka kuweka wazi ugonjwa uliokuwa unamsumbua.
0 comments:
Chapisha Maoni