test

Jumapili, 24 Mei 2015

KITANDA CHA MAMA MWENYE NYUMBA - 11


KITANDA CHA MAMA MWENYE NYUMBA -11
SEHEMU YA KUMI NA MOJA

IIPPOISHIA
“Ipi tena hiyo bosi?” aliuliza Helena. Akilini aliwaza kwamba, neno litakalotoka kwenye kinywa cha baba Joy ni…

“Mimi nimetokea kukupenda sana, sasa kwa sababu mama Joy analeta mambo ya kijinga naomba sana uwe mpenzi wangu, lakini tufanye kwa siri.”

Lakini kilichotoka kinywani mwa baba Joy ni hiki…

“Najua mzoa taka bado anaingia…na najua kwamba anapoingia wewe huwa unaona kwa macho yako. Sasa nataka nikupe pesa, lengo langu akiingia tu, unibip kwa simu, sawa?”

“Sawa bosi, lini…?”

“Leo, kesho, keshokutwa, yaani akija tu…”

“Sawa bosi…”

“Unataka shilingi ngapi?” baba Joy alimuuliza Helena huku akiwa amemkazia jicho la kusikiliza…

“Mh! Bosi, mimi nadhani angalia wewe mwenyewe kiasi utakachotaka kunipa sawa tu kwangu.”

“Oke, nikiwa natoka kwenda kazini nitakupa mzigo wako.”

“Sawa bosi.”

Baba Joy aliondoka hadi getini…

“Fuko…”

“Shikamoo bosi…”

“Achana na shikamoo, nataka tuongee…”

“Sawa bosi…”

“Naamini mzoa taka anapoingia wewe huwa unakuwa getini?”

“Ni kweli bosi, lakini…”

“Sitaki kujitetea, subiri nimalize ninachotaka kuongea…”

“Sawa bosi…”

“Nitakupa pesa, ninachotaka ni kwamba, akiingia tu, unanibipu…”

“Tena leo lazima atakuja bosi…”

“Una uhakika..?”

“Ndiyo bosi…”

“Oke, basi mimi nitakapotoka, nitajifanya nakwenda ofisini, lakini sitafika huko, nitakuwa jirani tu…”

“Sawa bosi.”

Baba Joy alirejea ndani, chumbani, akaenda kuoga. Wakati anaoga mama Joy aliamka na kutoka. Alianzia jikoni na baadaye uani. Alikuwa hajui hili wala lile…

“Nimemmisi mzoa taka wangu. Kale kakijana sijui kanatumia mzizi, nakapenda sana kuliko mlinzi. Ila Bonny yeye ana mwili wa mazoezi, amevimbavimba vizuri…teh… teh… teh teh!”

Baba Joy alipomaliza kujiandaa, alitoka mkononi ameshika brifkesi yake. Alianzia jikoni kwa Helena. Alipofika, aliweka brifkesi juu ya kabati na kulifungua, akatoa shilingi laki mbili…

“Kamata hizi Helena, nataka kazi nzuri…”

“Jamani bosi, asante sana, kazi njema,” alisema Helena huku akipokea kwa kuonesha dalili ya kupiga magoti.

Baada ya baba Joy kuondoka, mama Joy alitokea jikoni…

“Nimekusikia ukisema jamani bosi, asante sana, kazi njema, ni kitu gani amekupa?”

Helena alipigwa butwaa, akawaza haraka na kupata jibu kwamba, kama hakukiona alichopewa, hakuna haja ya kumtajia…

“Hajanipa kitu…”

“Sasa ulikuwa unashukuru nini..?”

“Alikuwa ameniaga kwamba anakwenda kazini nibaki salama ndiyo na mimi nikamwambia asante kazi njema.”

Mama Joy alitaka kukubali japo hakutoa sauti, akatoka kwenda mbele ya nyumba. Ile anatokea, akaona mkono wa mumewe ukitoka kama kushikana na mlinzi…

“Khaa! Toka lini baba Joy akasalimiana na mlinzi kwa kushikana mikono?” alijihoji mama Joy, naye akawa anaelekea usawa uleule. Alifika wakati mumewe akiwa ameshatoka na geti limeshafungwa na mlinzi…

“Leo baba Joy amekusalimia kwa kukupa mkono?”

“Ndiyo bosi…”

“Au alikuwa anakupa kitu?”

“Sijakiona bosi…”

“Hujakiona kinini?”

“Hicho kitu ulichosema alinipa.”

Mama Joy akaona kama anaongea na chizi, akarudi zake ndani na kuendelea na shughuli nyingine za kifamilia.

Mlinzi aliingia ndani ya kibanda chake na kuzihesabu zile pesa alizopewa na bosi wake…

“Kumi, ishirini, thelathini, aro…baini, haaamsiniii, sitini, sabini, themanini…” mlinzi alihesabu hadi alipokoma kwenye noti ya mwisho akiwa anatamka laki mbili…

“Duuu, ole wake aje leo mzoa taka, kitamnukia. Hii ndiyo mipango ya mjini bwana, kula na wewe uliwe, ala!” alisema kwa sauti mlinzi licha ya kwamba alikuwa pake yake.

Mara simu ya getini ilipigwa kutokea ndani, akaiwahi kuipokea…

“Haloo…”

“Fuko, akija mzoa taka mlete ndani moja kwa moja…”

“Sawasawa bosi.” Simu ikakata…

“Imekula kwako leo, utakiona cha mtema kuni,” mlinzi alisema moyoni.

Mpaka inatimu saa sita na nusu, mzoa taka alikuwa hajatokea. Na kwa usongo siku hiyo, kila mara mlinzi alikuwa akitoka getini na kuangaza kulia na kushoto.

Saa saba, baba Joy alimpigia simu Helena lakini hakuipokea kwa sababu mama Joy alikuwa beneti…

“We simu yako si inaita, kwa nini hupokei?”

“Ni msumbufu mtu mwenyewe…”

“Ni nani kwani?”

“Ni mtoto wa baba’angu mkubwa.”

Baba Joy alipoona simu ya Helena haipokelewi akampigia mlinzi wake…

“Bosi, mzoa taka hajatokea…”

“Ngo ngo ngooo,” geti liligongwa…

“Hebu subiri, geti linagongwa si ajabu yeye,” alisema mlinzi na kukata simu. Alikwenda kwenye geti dogo na kufungua akachungulia nje…

“Karibu bwana mzoa taka, karibu sana,” siku hiyo mlinzi alimchangamkia sana kuliko siku nyingine yoyote ile…

“Asante sana, nimekuja…”

“Eee, najua umekuja, demu wako alisema ukija nikupeleke mpaka ndani…”

“Demu wangu?”

“Aaa, sasa kwani bosi wangu si demu wako…”

“Acha hizo wewe, ingia twende,” Fuko alisema na kumshika mkono kwenda naye. Alipomfikisha ndani, mlinzi alirudi mbio getini na kuchukua simu yake kumpigia baba Joy…

“Simu unayoipiga kwa sasa haipatikani, tafadhali jaribu tena baadaye,” simu ilijibu hivyo. Alirudia na kurudia lakini majibu yakawa hayohayo.

Mara, Helena alitua getini.

“Fuko…”

“Naam…”

“Una namba nyingine ya bosi…?”

“Sina, unamtafuta..?”

“Sikiliza, aliniambia akija mzoa taka nimpigie simu, yeye hatakuwa mbali na maeneo haya, sasa simpati…”

“Hata mimi hivyohivyo, wewe alikupa na ‘hela’..?”

“Kwani wewe hajakupa hela..?”

“We nijibu kwanza mimi na mimi nitakujibu wewe…”

“Hamna, nijibu kwanza wewe,” alisema Fuko.

Wakati wao wakibishana kama walipewa fedha au la, mama Joy na mzoa taka walikuwa chumbani, walikaa kitandani wakisema wanaongea mambo yao…

“Mpenzi, chumba kimepatikana…”

“Wapi..?”

“Kule maeneo ya nanihi, si mbali sana…”

“Bonge la chumba. Simenti chumba chote, kikubwa kama uwanja wa mpira, halafu bei ya ubwete…”

“Ngoja kwanza, una maana mimi nitaweza kuja na gari nikaegesha mahali..?”

“Mh! mh! Mwenye nyumba anaweza kutengeneza pakingi ana nafasi kubwa…”



***

Baba Joy alikuwa amekaa kwenye mgahawa mmoja mpya. Hauna watu wengi na uko mtaa wa pili kutoka nyumbani kwake. Simu yake iliisha chaji na alikuwa akipigania kuchajiwa na mwenye mgahawa huo…

“Chaja ya pini ndigo ilikuwepo mzee, sijui nani kaichukua? We Benadi…” Benadi ni mhudumu wa mgahawa huo…

“Nani kachukua chaja ya pini ndogo..?”

“Sifahamu bosi, muulize Malinda jana alikuwa analalamika simu yake haina chaji,” alijibu Benadi.

Baba Joy alitoka mbio hadi nyumba ya pili baada ya mgahawa huo. Nyumba ambayo hakuna anayemjua…

“Jamani hodi…”

“Karibu,” binti mmoja, mweupe, mnene kiasi alitoka na kumwangalia kwa tabasamu mzee huyo…

“Karibu sana…”

“Asante…”

“Shikamoo…”

“Marhaba, shida yangu chaja, nipo kwenye mgahawa huo na kuna mtu wa muhimu sana natakiwa kumpigia, simu imeisha chaji.”

Yule binti alinyoosha mkono ili aipokee simu hiyo huku akisema…

“Au ulitaka chaja ukachajie hapo mgahawani..?”

“Ndiyo maana yangu, itakuwa si mbaya sana,” baba Joy alisema huku akionesha dalili za kuchanganyikiwa. Alimini kuwa, endapo ataiacha simu yake pale ndani akipigiwa na Helena au Fuko hatajua.

Yule binti aligeuka kurudi ndani akimaanisha anakwenda kuchukua chaja. Baada ya muda alirejea…

“Hii, si utairudisha mwenyewe..?”

“Usajali binti, nitairudisha mimi mwenyewe, nakushukuru sana binti yangu…”

“Usijali baba.”

Baba Joy alitoka haraka na chaja hiyo hadi kwenye ule mgahawa…

“Ee bwana nimebahatisha chaja, naomba nichomekee kwenye soketi yenu basi.”


JE NINI KITAENDELEA ...USIKOSE...SEHEMU YA ....12...

Install Application ya JUNGUKUULEO Uweze Pata Habari Kirahisi Zaidi

xxxxxxxxxxxxx

0 comments:

Chapisha Maoni