Filimbi ya kuanzisha mbio za urais kwa tiketi ya CCM itapulizwa Mei 23 baada ya kumalizika kwa kikao cha Halmashauri Kuu ya chama hicho tawala, huku makada sita walio ‘kifungoni’ wakitarajia kujua hatima yao kwenye mbio hizo Mei 20.
CCM imekuwa kimya kuhusu mchakato wake wa
uchaguzi, unaohusisha ratiba ya chama hicho, kupitishwa kwa Ilani ya
Uchaguzi na taratibu nyingine za kugombea uongozi, kiasi cha kutia
wasiwasi baadhi ya wanachama wake, wakiwamo makada sita ambao
walifungiwa kwa zaidi ya miezi 12 kujihusisha na kuwania madaraka baada
ya kubainika kukiuka taratibu.
Makada hao waliopewa adhabu na Kamati Kuu ni
mawaziri wakuu wa zamani, Edward Lowassa na Frederick Sumaye na Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.
Wengine Steven waziri, ambaye ni Waziri wa Kilimo
na Chakula, January Kamamba (Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia) na
William Ngeleja, ambaye alikuwa Waziri wa Nishati na Madini.
Mbali na makada hao, Naibu Katibu Mkuu wa CCM,
Mwigulu Nchemba aliwahi kupewa barua ya katazo la kufanya ziara na
mikutano ya kibinafsi yenye viashiria vya kampeni za urais.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye
hakutaka kuthibitisha kuwapo kwa vikao vya vyombo hivyo viwili wiki
mbili zijazo.
“Kwanza habari hizo siyo za kweli, nazisikia kwa
mara ya kwanza kutoka kwako,” alisema Nape alipoulizwa kuhusu tarehe za
vikao hivyo.
“Kwanza umeshaandika stori yenu halafu ndiyo
mnanipigia kuthibitisha. Inakuwaje msemaji wa chama hana habari, halafu
nyinyi Mwananchi muwe nazo?” alihoji Nape.
Hata hivyo, habari za uhakika ambazo Mwananchi
imezipata zinaeleza kuwa Kamati Kuu ya CCM itakutana Mei 20, kuandaa
taratibu zote za uchaguzi na siku inayofuata, yaani Mei 21 iwasilishe
kwenye kikao cha Halmashauri Kuu kitakachokuwa cha siku mbili.
Habari hizo zinaeleza kuwa vikao hivyo viwili
vinatarajiwa kutoa ratiba na utaratibu wa kuchukua na kurudisha fomu kwa
waombaji wa nafasi za udiwani, ubunge na urais na kupokea na kupitisha
ilani ya uchaguzi ya chama hicho.
Chanzo cha habari kutoka ndani ya CCM kimelieleza Mwananchi kuwa vikao hivyo vitahitimisha suala la wagombea sita wa
urais waliopewa onyo kali kwa kuanza kampeni mapema na kushiriki vitendo
vya utovu wa nidhamu.
Habari kutoka ndani ya CCM pia zinaeleza kuwa
katika eneo la mchakato ripoti za Kamati Ndogo ya Maadili, chini ya
makamu mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula itatikisa vikao hivyo hasa
uchunguzi wake kuhusu mienendo na harakati za kuwania urais.
Wasiwasi na shauku ya ripoti ya kamati hiyo inatokana na kauli
za hivi karibuni za Mangula kuwa chama hicho kinazo taarifa za makundi
ya makada wanaosaka urais na matumizi makubwa ya fedha.
Makada hao, ambao miongoni mwao wanapewa nafasi
kubwa ya kupitishwa kupeperusha bendera ya CCM kwenye mbio za urais,
walidaiwa kukiuka taratibu inayozuia wanachama kuanza kampeni mapema na
adhabu yao ilitakiwa imalizike Februari mwaka huu, lakini ikaongezwa kwa
maelezo kuwa Kamati ya Maadili bado inaendelea na uchunguzi.
Mbali na makada hao sita, wengine wanaotajwa kuwa
na nia ya kuchukua fomu ni aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la
Kujenga Taifa, Emmanuel Nchimbi na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani,
Shamsi Vuai Nahodha ambao jana walitangazwa kusafishwa dhidi ya tuhuma
za kutowajibika katika Operesheni Tokomeza.
Wawili hao walilazimika kuachia ngazi mapema mwaka jana baada ya Kamati ya Bunge kutoa taarifa ya uchunguzi wake kuhusu ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu uliokuwamo kwenye operesheni hiyo iliyolenga kupambana na ujangili.
Wawili hao walilazimika kuachia ngazi mapema mwaka jana baada ya Kamati ya Bunge kutoa taarifa ya uchunguzi wake kuhusu ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu uliokuwamo kwenye operesheni hiyo iliyolenga kupambana na ujangili.
Vilevile, vikao hivyo vinatarajiwa kupokea na kujadili mapendekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa kipindi cha 2015-2020.
Vyanzo vingine vya habari vimeeleza kuwapo pia kwa
ajenda ya hali ya siasa inayohusishwa na misuguano ndani ya chama bara
na visiwani, uandikishaji wapigakura, mchakato wa Katiba mpya na jinsi
ya kupambana na wapinzani, hasa Ukawa.
Kamati Kuu inatarajia kutumia vikao hivyo
kuangalia namna ya kupata wagombea watakaokubalika kwa wananchi kuelekea
kwenye kinyang’anyiro cha urais, wabunge na madiwani.
Chanzo: Mwananchi
Chanzo: Mwananchi
0 comments:
Chapisha Maoni