KIJANA
wa Kitanzania, Shujaa Suleiman Shujaa ameibuka kidedea na kitita cha
sh. milioni 15 katika mashindano ya 19 ya Afrika ya kuhifadhi Quran
kwenye kundi la washiriki wa juzuu 30.
Shujaa
mwenye miaka 23 ambaye ni mkazi wa Morogoro, amejishindia pia laptop,
kiwanja chenye hati eneo la Kigamboni kilichotolewa na kampuni ya
Property International ya jijini Dar es Salaam pamoja na dola za
Marekani 500 kutoka kwa Bw. Ahmed Seif “Magari” aliyetoa dola 500 kwa
washindi wote watano.
Akizungumza
na maelfu ya waumini na Watanzania waliofurika kwenye Uwanja wa Taifa
jijini Dar es Salaam jana mchana (Jumapili, Mei 27, 2018), Waziri Mkuu
Kassim Majaliwa amewataka Watanzania waendelee kuilinda amani iliyopo
nchini kwani ikipotea hakuna atakayeweza kufanya ibada.
“Mtakubaliana
nami kuwa amani ya nchi yetu, ndiyo inatufanya tutembee vifua mbele
dhidi ya wenzetu, ni neema kubwa ambayo kila muumini anapaswa kuilinda
kwani ikipotea hata mkusanyiko wetu huu wa leo si rahisi kufanyika
mahali kama hapa,” alisema.
“Leo
hii tuko hapa uwanjani kwa sababu tuna amani, kama Serikali isingekuwa
inashirikisha Watanzania wote kulinda amani, basi tusingeweza kukutanika
hapa. Kuna nchi 18 ziko hapa, na watu wake wamekuja hapa uwanjani kwa
kuwa wana uhakika na amani tuliyonayo sisi Watanzania,” alisema.
Alisema katika nchi ambazo amani imetoweka, watu wanalazimika kufanya shughuli za ibada majumbani au kwa kujificha.
“Wenzetu
hao, hawapati fursa adhimu kama hii ya kujumuika pamoja na majirani,
ndugu, jamaa na marafiki kusikiliza na kufurahia kisomo cha Quran au
kufanya shughuli nyingine za kiuchumi na kijamii,” aliongeza.
Aliwataka
Watanzania waendelee kubeza na kupuuza kauli za walio wachache ambao
kwao kuzungumzia amani ni kujipendekeza kwa Serikali. “Watu hao
wamesahau kwamba tofauti katika Uislamu hazikuanza leo, lakini tofauti
hizo hazikuwa sababu ya wema waliotangulia kuacha kuheshimiana na
kushirikiana,” alisisitiza.
Mshindi
wa pili kwenye kundi hilo la juzuu 30 ni Ahmed Noor wa Sudan ambaye
ameshinda sh. 12,564,750 pamoja na laptop akifuatiwa na Muzamil Awadh
Mohamed wa Sudan alijishindia sh. milion 7.5 pamoja na laptop
zilizotolewa na kampuni ya Camara Education.
Mshindi
wa nne ni Abdulally A. Mohammed wa Kenya aliyepata zawadi ya sh.
5,711,000 na wa tano ni Ibrahim Maazur kutoka Niger, aliyepata sh.
3,426,000. Washindi hao wote watano walipewa zawadi ya kwenda hijja na
Waziri wa Mambo ya Dini wa Saudi Arabia, Dk. Saleh Ally Sheikh.
Washiriki
wengine kwenye kundi la juzuu 30 walitoka nchi za Rwanda, Burundi,
Msumbiji Djibouti, Kenya, Ethiopia, Congo DRC, Nigeria, Ghana na Afrika
Kusini.
Washiriki
wengine waliopewa zawadi ni wale walioweza kuhifadhi Juzuu tatu
(washindi watatu), Juzuu tano (washindi watatu); Juzuu 10 (washindi
watatu) na Juzuu 20 (washindi watatu).
Viongozi
wengine waliohudhuria mashindano hayo ni Makamu wa Rais Mstaafu wa
awamu ya nne, Dk. Mohammed Gharib Billal, Katibu Mkuu wa CCM,
Abdulrahman Kinana na mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa Tanzania
kutoka Saudi Arabia, Comoro, Oman, Uturuki, Kenya, Msumbiji na Nigeria,
Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir bin Ally na
Rais wa taasisi ya Al-Hikma, Sheikh Sharif Abdilkadir Al-Ahdal.
Katika
hatua nyingine, Waziri Mkuu amemtaka Sheikh Nurdin Mohammed Ahmad
(maarufu kama Sheikh Kishki) akaonane na Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi, Bw. William Lukuvi ili atoe maamuzi ya kiwanja chao
kilichopo eneo la Matumbi ambacho mwaka jana aliagiza kifuatiliwe
taratibu zake na kisha wapatiwe.
“Kuhusiana
na suala la kiwanja mlichosema, mamlaka ya awali ni Manispaa ya Temeke
na ilishakamilisha taratibu zote za kisheria, ikapeleka kwa Afisa Ardhi
wa Mkoa kuona kama limepita kwenye vikao vyote ndipo wanaenda wizarani
kupata kibali. Hakuna sababu ya wizara kuikatalia manispaa huku eneo
lenyewe likiwa kwenye ramani kuu ya manispaa yenyewe, nenda mumuone
Waziri mwenye dhamana, awape ardhi,” alisema.
Waziri
Mkuu amefikia hatua hiyo baada ya kupewa taarifa akiwa jukwaani kwamba
taasisi ya Al-Hikma iliwasiliana na Manispaa ya Temeke, hadi mkoani
wakapewa barua zinaonyesha eneo liko sawa lakini walipofika wizarani
wamekwamishwa na Afisa mmoja aliyemtaja kwa jina moja la Mama Mpetula.
Juni
11, mwaka jana katika mashindanio ya 18, taasisi ya Al-Hikma waliomba
wapatiwe kiwanja na.118 kwenye kitalu E kilichoshikamana na kiwanja na.
117 chenye shule yao ya Al-Hikma Girls iliyoko Temeke ili waweze kujenga
zahanati.
0 comments:
Chapisha Maoni