Mkurugenzi
wa Facebook Mark Zuckerberg ameomba msamaha kwenye Bunge la Ulaya
kutokana na madhara yaliyosababishwa na kuvuja kwa data za watumiaji wa
mtandao huo na pia kwa kushindwa kupambana na habari za uongo/ feki.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Facebook Mark Zuckerberg aliomba msamaha kwa watumiaji wa
Ulaya wa mitandao ya kijamii na kuahidi kupambana na habari feki za
uongo na vile vile ameahidi kwamba data za watumiaji hao zitalindwa
vyema.
Zuckerberg
alifika mbele ya viongozi wa makundi ya kisiasa wa Bunge la Ulaya baada
ya Facebook kukubali kwamba ilitoa taarifa binafsi za watumiaji wapatao
milioni 87 kwa kampuni ya Cambridge Analytica ya nchini Uingereza,
zikiwemo zile za watumiaji karibu milioni 2.7 kutoka kwenye nchi za
Umoja wa Ulaya. Facebook ilikubali kwamba ilitoa taarifa hizo binafsi
kwa njia isiyo sawa.
Hata
hivyo Zuckerberg aliyakwepa baadhi ya maswali magumu aliyoulizwa na
wabunge hao, na kisha kuomba msamaha kutokana na sera za Facebook
zilizorahisisha kuenea kwa habari feki wakati wa uchaguzi wa rais wa
Marekani wa 2016 na pia katika matokeo ya kura ya maoni juu ya Uingereza
kujiondoa kutoka Umoja wa Ulaya.
Baadhi
ya wabunge wa Umoja wa Ulaya hata hivyo wamelalamika kwamba Zuckerberg
hakutoa majibu halisi juu ya matumizi mabaya ya data za mamilioni ya
watumiaji wa mtandao huo.
Jan
Philipp Albrecht, mjumbe maalum wa Umoja wa Ulaya anayeshughulikia
ulinzi wa data za Umoja huo (GDPR) amesema ipo haja ya kuwepo ulinzi
mkubwa.
Mjumbe
huyo maalum anayeshughulikia masuala ya ulinzi wa data katika Umoja wa
Ulaya amesema pia uangalizi unahitajika zaidi kwenye shughuli za mtandao
huo wa Facebook, kwa mfano katika kuitenganisha Facebook na WhatsApp au
Facebook Messenger ambapo hatua kama hiyo sasa itakuwa ni chaguo la mtu
binafsi . Bwana Albrecht amesema hilo ni moja kati ya maswali ambapo
Mark Zuckerberg hakutoa majibu ya kina.
Zuckerberg
ameomba msamaha kwa niaba ya kampuni yake kwa kushindwa kuzuia kutumiwa
vibaya baadhi ya mifumo yake ya internet huku wengi wa wabunge
waliokuwepo katika mahojiano hayo wakisema bilionea huyo wa Facebook
alishindwa kutoa majibu yaliyoweza kuwatoa wasiwasi walio nao.
Mfumo
wa kujibu maswali ulimruhusu Zuckerberg kujibu maswali hayo mwishoni,
na hivyo kuwaacha wabunge wakiwa wamekata tamaa kutokana kushindwa
kupata majibu ya moja kwa moja kwa maswali yao.
Rais
wa Bunge la Ulaya Antonio Tajani alimwambia Zuckerberg kwamba kufika
kwake kumetoa ishara muhimu ya heshima yake kwa Bunge hilo pamoja na
wananchi wa Ulaya.
0 comments:
Chapisha Maoni