Rais
wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Tundu Lissu anayemaliza muda
wake amewaaga wanachama wa chama hicho huku Jaji Kiongozi, Ferdinand
Wambali akieleza kuwa wanafanya kila linalowezekana kukomesha rushwa
kwenye mfumo wa sheria.
Jaji Wambali akifungua mkutano mkuu wa TLS jana, alisema rushwa inawanyima haki wananchi.
Aliwataka
wanasheria kujitathmini kama malengo ya kuanzishwa taasisi hiyo
yanaakisi shughuli zao sasa kulinganisha na idadi kubwa iliyopo ya
wanasheria.
Alisema
katika kuharakisha huduma za kisheria, mfumo wa Mahakama umeboresha
utendaji kazi kwa kutumia teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama)
ili kusaidia upatikanaji wa haki kwa haraka.
Lissu
akiwa nchini Ubelgiji anakoendelea na matibabu, aliwaandikia wanachama
wenzake barua ya kuwaaga akisema; “Jioni ya Machi 18 mwaka jana,
nilisimama mbele yenu na kutoa hotuba yangu nikiwa rais mpya. Juni 30,
2017 nilizungumza nanyi tena Dar es Salaam katika mkutano wa dharura wa
TLS, lakini leo nazungumza nikiwa katika kitanda cha Hospitali ya
Ubelgiji nikiuguza majeraha kama mnavyojua.”
Katika
salamu hizo zenye kurasa 10, Lissu ameelezea tukio la Septemba 7 mwaka
jana, aliposhambuliwa na watu wasiojulikana kwa risasi zaidi ya 38 akiwa
nyumbani kwake mjini Dodoma kisha kusafirishwa kwenda Hospitali ya
Nairobi kabla ya kwenda Ubelgiji.
“Mlinipa
nafasi ya kuwahudumia kwa kipindi cha mwaka mmoja lakini kipindi hicho
kilikatishwa miezi saba,” alisema Lissu huku akielezea kwa ufupi
mafanikio aliyoyafanya kwa muda huo.
Lissu
ambaye pia ni mbunge wa Singida Mashariki (Chadema) amezungumzia
masuala mbalimbali huku akiwataka wanasheria hao kupigania utawala wa
sheria kwani bila kufanya hivyo hali itakuwa mbaya na hakuna atakayekuwa
salama.


0 comments:
Chapisha Maoni