SAA
chache baada ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuagiza kusitishwa kwa
mpango wa uuzaji shamba la Lerongo linalomilikiwa na Chama Kikuu cha
Ushirika mkoani Kilimanjaro (KNCU), ili kuokoa benki yake isinyang'anywe
leseni na kufungwa, vigogo wa chama hicho wanaumiza vichwa kutafuta
njia mbadala.
Sasa
bodi ya wakurugenzi ya KNCU inakutana leo kujadili katazo hilo na
kutafuta mbinu mpya ya kuiwezesha Benki ya Ushirika Kilimanjaro (KCBL)
kukidhi masharti ya hitaji la kisheria ya kufikisha mtaji wa Sh. bilioni
tano.
Mwenyekiti
wa KNCU, Aloyce Kitau alithibitisha jana kwamba tayari ameitisha kikao
cha bodi ya wakurugenzi kujadili hatima ya KCBL baada ya Waziri Mkuu
kusitisha mchakato wa kuuza ekari 581 za shamba la Lerongo lililopo
Wilaya ya Siha.
"Kwa ujumla tume-paralize (tumepooza) baaada ya amri hiyo ya PM (Waziri Mkuu)," alisema Kitau kwa njia ya simu jana.
"Kwa
jinsi hali ilivyo na masharti yaliyowekwa na Benki Kuu, nimeitisha
kikao cha bodi ya wakurugenzi kesho (leo) kutafuta mbinu mpya za
kuinusuru benki yetu ya KCBL kabla ya deadline (muda wa ukomo)
haijapita.
"Unajua
serikali ndio Mungu wa duniani kwa hiyo hatuwezi kubishana nayo,
tumepokea taarifa hiyo na tunatafuta sasa plan B (namna nyingine)
kukidhi takwa la kufikisha mtaji wa Sh.bilioni tano."
KCBL
inakabiliwa na upungufu wa mtaji, tatizo ambalo hualika BoT
kunyang'anya leseni na kufungia benki husika, ikiwamo tano kwa pamoja
mwanzoni mwa mwezi huu.
Aidha,
benki hiyo ambayo inamilikiwa na KNCU kwa asilimia 69, inahitaji kiasi
cha Sh. bilioni tano, ili kufikisha mtaji wa Sh. bilioni 6.5
ulioelekezwa na BoT uwe umefikiwa hadi ifikapo Juni, mwaka huu.
Uamuzi
wa kuuza shamba hilo ulitangazwa Jumanne na Mwenyekiti Kitau wakati
akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mkakati wa kuinusuru benki
hiyo isifutiwe leseni.
Kitau
aliwasihi wananchi wa mkoa wa Kilimanjaro kuendelea kutumia benki hiyo
kwani hadi kufikia Jumanne michakato yote na kibali cha kuuza shamba
hilo ilikuwa imekamilika, na kwamba KCBL ingefikia mtaji husika kama
inavyotakiwa kisheria mapema iwezekanavyo.
0 comments:
Chapisha Maoni