Jaji
Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewataka Watumishi wa
Mahakama nchini kutoa huduma kwa kuzingatia Maadili, kuhakikisha kesi
zinamalizika kwa wakati pamoja na kuacha vitendo vya rushwa ili kuongeza
imani ya wananchi kwa Mhimili huo.
Akizindua
wiki ya Sheria na Maonesho ya Elimu ya Sheria jana katika viwanja vya
Mnazi Mmoja jijini Dar es salaam, Jaji Mkuu alisema kuwa nguvu ya
Mahakama ni imani ya wananchi na imani hiyo itaongezeka ikiwa hakuna
rushwa, kuna maadili mema na kesi zitamalizika kwa wakati.
Jaji
Mkuu pia amewataka wananchi kuacha kuilalamikia Mahakama na badala yake
wachukue hatua kwa kuwataja watumishi wasiozingatia maadili kwa uongozi
wa Mahakama.
Aidha,
amewashauri wananchi kujifunza na kuelewa taratibu za mashauri
Mahakamani ili kurahisisha upatikanaji wa haki zao wanapozitafuta kwenye
Mahakama mbalimbali nchini.
“Wananchi
wengi wanakwenda kutafuta haki sehemu isiyohusika hivyo wanatakiwa
kujifunza taratibu za Mahakama ili waweze kupata haki kwa wakati kwa
kuwamuda mwingi unapotea kwa kutafuta haki mahali pasipostahili”,
alisema Prof. Juma.
Alisema
hivi sasa Mahakama inaingia kwenye matumizi ya Teknolojia ya habari na
Mawasiliano- TEHAMA hivyo matumizi haya yatamsaidia mwananchi kuweza
kufahamu hatua zote za shauri lake lililopo Mahakamani.
Jaji
Mkuu ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi katika viwanja vya
Mnazi Mmoja ili kupata elimu juu ya masuala mbalimbali yanayohusu
Mahakama na sekta ya sheria kwa ujumla.
Alisema,
katika maonesho hayo, wananchi watapata nafasi ya kujifunza juu ya
usuluhishi nje ya Mahakama, Mahakama inayotembea (Mobile Courts) pamoja
na changamoto za upatikanaji wa haki zikiwemo upungufu wa Watumishi,
Miundombinu, pamoja na vifaa.
Akizungumzia
taratibu wa usuluhishi wa kesi nje ya Mahakama (Mediation), Jaji Mkuu
amesema wakati sasa umefika kwa wananchi kutumia utaratibu huo
unaorahisisha upatikanaji wa haki na kuongeza kuwa Haki bora hupatikana
kwa usuluhishi majumbani.
Aidha,
kabla ya kuzindua wiki ya Sheria, Jaji Mkuu aliongoza Matembezi
waliyowashirikisha watumishi wa Mahakama, wadau pamoja na wananchi kwa
ujumla yaliyoanzia katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mpaka viwanja
vya Mnazi Mmoja.
Matembezi
hayo pia yalihudhuriwa na viongozi wa Serikali akiwemo Waziri wa wakati
katiba na Sheria Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi, Katibu Mkuu wa wizara
hiyo Prof. Sifuni Mchome pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya
Katiba na Sheria, Amon Mpanju.
0 comments:
Chapisha Maoni