test

Jumanne, 31 Oktoba 2017

Uhuru Kenyatta Atangazwa Mshindi Wa Urais Nchini Kenya Kwa Asilimia 98


Hatimaye Tume ya Taifa ya Uchaguzi (IEBC) imemtangaza Uhuru Kenyatta kuwa mshindi wa kinyang’anyiro cha urais baada ya kujikingia kura 7,483, 895 sawa na asilimia 98 katika uchaguzi wa marudio uliosusiwa na mpinzani wake mkuu, Raila Odinga.
 
Kwa matokeo hayo, Rais Kenyatta na makamu wake William Ruto walikabidhiwa vyeti vya ushindi na sasa Uhuru anasubiri kuapishwa kuiongoza nchi kwa miaka mitano ikiwa matokeo hayo hayatapingwa na kufutwa.
 
Mwenyekiti wa IEBC, Wafula Chebukati alitangaza matokeo hayo bila kura kutoka majimbo 25 ya eneo la Nyanza ambalo wafuasi wa Odinga walifanya vurugu na kusababisha uchaguzi kuahirishwa.
 
Chebukati alisema mazingira yaliyokuwa yameandaliwa kwa ajili ya uchaguzi wa marudio yaliwezesha kuwa wa kuaminika, huru na wa haki.
 
Akizungumza mapema, Makamu mwenyekiti wa IEBC Consolata Nkatha alisema kura za maeneo ambayo hayakufanya uchaguzi hayawezi kuathiri matokeo ya mwisho.

Nkatha alisema mchakato ulikamilika katika majimbo 266 ambako uchaguzi ulifanyika na kwamba tume, kwa kuzingatia kifungu cha 55(B)(3) cha Sheria ya Uchaguzi ambacho kilielekeza marudio kufanyika na hivyo kusafisha njia kwa rais mteule kutangazwa.
 
Alhamisi iliyopita, ulifanyika uchaguzi mpya wa marudio kama ilivyoamuliwa na Mahakama ya Juu katika uamuzi wa jumla Septemba Mosi uliobatilisha ushindi wa Rais Kenyatta wa Agosti 8 kwa madai ya kuwepo kasoro na dosari zilizofanywa na IEBC.
 
Odinga alisusia uchaguzi wa marudio akitaka, pamoja na mambo mengine wafukuzwe maofisa wa tume na mchapishaji wa makaratasi ya kura na msambazaji wa vifaa vya kiteknolojia.
 
Hata hivyo, ilikuwa vigumu kuandaa uchaguzi katika majimbo 25 Kisumu, Siaya, Homa Bay na Migori ambako Odinga anaungwa mkono.
 
Katika majimbo mengi, uhuni ulikithiri kiasi cha kuzuia kabisa upigaji kura wa marudio kwani walifunga mageti na kuchomelea kwa nondo na wengine walizusha ghasia kiasi kwamba IEBC ilishindwa kuwalinda maofisa wake.
 
Chebukati alisema Ijumaa iliyopita kwamba maofisa wa uchaguzi walitishwa, walitekwa au kuteswa na akasema ilitilia maanani sana kokote ambako maofisa wake walikabiliwa na vitisho.

Uchaguzi ulifanyika katika majimbo 265 kati ya 290 ya Kenya yakiwemo ya nje ya nchi ambapo Wakenya waishio Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika walipiga kura.
 
Katika majimbo 266 Rais Kenyatta alipata kura 7,483, 895 yaani kura 719,395 chini yakura 8,203, 290 alizopata katika uchaguzi uliofutwa.
 
Kwa kura 7,616, 21 halali zilizopigwa katika majimbo 266 yaliyoshiriki uchaguzi, idadi hiyo ni sawa na asilimia 42.36 wakati ikipigiwa hesabu kwa watu 19, 611, 423 waliojiandikisha walioshiriki uchaguzi wa Alhamisi walikuwa asilimia 38.84.
 
Uchaguzi wa Agosti 8 waliojitokeza walikuwa asilimia 79.17 idadui ambayo ilikuwa pungufu ikilinganishwa na mwaka 2013 waliposhiriki asilimia 86 ambao Kenyatta alimshinda Odinga katika kinyang’anyiro kikali. Odinga alipinga matokeo lakini alishindwa Mahakama ya Juu.

Install Application ya JUNGUKUULEO Uweze Pata Habari Kirahisi Zaidi

xxxxxxxxxxxxx

0 comments:

Chapisha Maoni