Ofisi
ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imetangaza
kutoa vibali vya ajira 10,184 ili kuziba nafasi zilizoachwa wazi na
watumishi wa umma waliobainika kughushi vyeti vya elimu, imefahamika.
Kwa
mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano
Serikalini Ofisi ya Rais, Utumishi, Florence Temba, ilieleza kuwa agizo
hilo linazihusu Mamlaka za Serikali za Mitaa, Sekretarieti za Mikoa,
Wakala wa Serikali, pamoja na Taasisi na Mashirika ya Umma.
Ilimnukuu
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, Angela Kairuki akitoa agizo hilo wakati akizungumza katika
kikao kazi na watumishi wa Umma wa Wilaya ya Kigamboni mkoani Dar es
Salaam jana.
“Mgawanyo
wa vibali vya ajira umezingatia upungufu uliojitokeza baada ya
kukamilika kwa zoezi la uhakiki, vipaumbele vya Taifa kwa sasa na
upatikanaji wa watumishi kutoka katika soko la ajira,” alisema Kairuki.
Kairuki
aliongeza kuwa taratibu za kukamilisha mgawo wa nafasi za ajira 4,816
zilizosalia unaendelea ili kuwezesha wizara na taasisi nyingine
zilizokamilisha uhakiki wa watumishi wa umma hivi karibuni kuajiri
watumishi wapya kuziba nafasi wazi zilizojitokeza.
Alieleza
kuwa serikali imetoa kibali kuajiri watumishi wapya 15,000 ili kuziba
pengo lililosababishwa na kuondolewa kwenye orodha ya malipo ya
mishahara kwa watumishi wa umma waliobainika kughushi vyeti baada ya
zoezi la uhakiki.
“Watumishi wa umma watakaoajiriwa kuziba nafasi hizo wanatarajiwa kuripoti kazini kuanzia mwezi Agosti, 2017,”
alieleza Waziri Kairuki, na kuongeza kuwa utaratibu wa ajira mpya za
serikali upo palepale na amewataka wananchi kutokuwa na wasiwasi wowote
wa ajira hizo.
“Napenda
kusisitiza kuwa vibali tulivyovitoa leo ni vile vilivyoziba pengo la
walioghushi vyeti, naomba wananchi watambue kuwa suala la ajira mpya
bado liko pale pale kama serikali ilivyojipanga,” alisema Kairuki.
Aprili
mwaka huu, Rais John Magufuli alipokea ripoti yenye orodha ya watumishi
wa umma ambao kati yao wanadaiwa kuwa na vyeti pungufu, vyenye utata na
vya kughushi kutokea kwa Waziri Kairuki.
Waliokuwa
na vyeti vya kughushi walikuwa 9,932, na Rais aliapa kwamba hawatarudi
kazini. Rais Magufuli aliagiza kufutwa kazi kwa wote waliotajwa kwenye
ripoti hiyo na kuzuia mishahara yao ya mwezi huo, lakini hata hivyo bado
mlango uliwekwa wazi kwa wenye pingamizi na wapo waliokataa rufaa huku
wengine wakienda kwenye mamlaka husika kutafuta ufumbuzi wa suala hilo.
Wiki
iliyopita akiwa Dodoma, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk Laurean Ndumbaro alitangaza kuwa
wiki hii serikali itatoa vibali 3,000 vya ajira katika sekta ya afya
vikiwemo vya madaktari na wauguzi pamoja na maofisa hesabu 535 kwa ajili
ya vituo vya afya vya kata ili washughulike na ukusanyaji wa mapato
kwenye vituo vya afya na zahanati.
0 comments:
Chapisha Maoni