Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imekusanya Sh trilioni 8.41 kuanzia Julai mwaka jana hadi Januari mwaka huu.
Taarifa
iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana na Mkurugenzi wa Huduma na Elimu
kwa Mlipakodi, Richard Kayombo, inaonesha makusanyo ya Januari mwaka
huu ni Sh trilioni 1.14.
Kayombo
alisema pamoja na juhudi za kukusanya kodi mbalimbali, hivi sasa
wameelekeza nguvu katika kukusanya kodi ya majengo kwa kutoa ankara kwa
wamiliki wa majengo katika mikoa mbalimbali.
“Wamiliki
wa majengo wanakumbushwa kwamba kodi ya majengo inakusanywa na TRA
kuanzia Julai mwaka jana, hivyo tunawaomba watoe ushirikiano kwa kulipia
ankara zao kwa wakati,” alisema Kayombo.
Kuhusu
zoezi la uhakiki wa Namba ya Mlipakodi (TIN), alisema kuna mafanikio
makubwa na kwamba wananchi wa mikoa ya Arusha, Mwanza, Kilimanjaro,
Dodoma, Mbeya, Morogoro, Tanga na Pwani waitikie wito huo mapema kuepuka
usumbufu.