test

Jumatatu, 27 Februari 2017

Rais Museveni Awakaribisha Watanzania Kuwekeza Nchini Uganda


 Na. Immaculate Makilika na Lilian Lundo- MAELEZO.
Rais wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Yoweri Museveni ametoa wito wafanyabiashara wa Kitanzania kwenda kuwekeza nchini Uganda.


Rais Museveni ametoa kauli hiyo leo wakati alipotembelea viwanda vya Kampuni ya Bakhresa vinavyozalisha Unga na Juisi vya Buguruni na Vingunguti jijini Dar es Salaam.

“Nawakaribisha wafanyabiashara wa Kitanzania kuja nchini Uganda kuwekeza kwani kufanya hivyo kutasaidia kuzalisha bidhaa, upatikanaji wa soko pamoja na ajira” alisema Rais Museveni.

Kauli hiyo ya Rais Museveni imetokana na mafanikio yanayotokana na Mwekezaji wa Kitanzania Said Salim Bakhresa aliyewekeza nchini Uganda ambapo anamiliki Kiwanda cha kusanga ngano nchini humo.

Kwa upande wa Mkurugenzi wa Mahusiano wa Kampuni za Bakhresa Hussin Sufiani amesema kwamba Kampuni hiyo iko mbioni kuongeza uzalishaji wa unga wa ngano kutoka tani 1,100 hadi kufikia tani 2,000 kwa siku nchini Uganda.

Aidha, amesema kutokana na uwekezaji wa Kampuni hiyo nchini Uganda jumla ya Waganda 650 wamenufaika na ajira mbalimbali ambazo zinasaidia kuwapatia kipato.

Kwa upande wa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe. Charles Mwaijage amesema kuwa Uganda na Tanzania zimeingia makubaliano ya ushirikiano katika sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya viwanda.

Amesisitiza Watanzania wanaweza kwenda kuwekeza nchini Uganda kwa vile nchi hiyo wanalima tani milioni 4 za mahindi lakini wana uwezo wa kutumia tani milioni moja pekee, hivyo ni fursa kwa wafanyabiashara wa Kitanzania kwenda kuwekeza nchini humo.

“Tunawahamasisha wafanyabiashara wa Uganda na Tanzania kuwekeza katika nchi zao ili kuzalisha , bidhaa na ajira za kutosha kwa wananchi” alisema Waziri Mwijage.

Waziri Mwijage alitoa Wito kwa Watanzania kushiriki katika uchumi wa viwanda kwa kufanya uzalishaji wa bidhaa zinazotumika viwanda mfanio kwa kulima matunda au mbogamboga.

Rais Yoweri Museveni aliwasili nchini jana kwa ziara ya kiserikali ya siku mbili ambapo akiwa nchini alifanya mazungumzo na Mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli na kutembelea Viwanda vya Said Salim Bakhresa vya Tazara na Vingunguti.

Install Application ya JUNGUKUULEO Uweze Pata Habari Kirahisi Zaidi

xxxxxxxxxxxxx