Mchezaji
wa zamani wa klabu ya Yanga, Prisons na Taifa Stars, Geofrey Bonny
'Ndanje' (37), amefariki dunia usiku wa kuamkia leo Jijini Mbeya
alikokuwa akipatiwa matibabu baada ya kusumbuliwa kwa muda mrefu na
maradhi ya kifua kikuu
Awali
taarifa za kuugua kwa kiungo huyo zilianza kusambaa kwenye mitandao ya
kijamii, watu wakichangishana pesa kwa ajili ya kumsaidia mchezaji huyo
kuendelea kupata matibabu katika hospitali hospitali ya Makandana -
Tukuyu wilayani Rungwe mkoani Mbeya.
Dada
wa mchezaji huyo aliyepewa nafasi katika timu ya Taifa Stas na kocha
Marcio Maximo, Neema amesema, wamempoteza kipenzi chao baada ya
kuhangaika naye kumuuguza kwa muda mrefu.
"Tumempoteza
ndugu yetu ambaye amefariki usiku wa kuamkia leo, sisi tumekwenda
majira ya saa 11:00 alfajiri tukakuta tayari amekwishafariki. Tumekuwa
tukimuuguza kwa muda mrefu lakini Mungu amepanga yake, msiba upo
nyumbani mjini Mbeya ambako taratibu za mazishi zimekwishaanza," amesema Neema Dada yake Marehemu Bonny.
Bonny
alikuwa mchezaji wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars enzi za
kocha Mbrazil, Marcio Maximo na wengi wanamkumbuka kwa soka lake
maridadi katika sehemu ya kiungo, licha ya kwamba aliibuliwa wakati umri
wake umekwishaenda.
Alicheza
Yanga chini ya kocha Mserbia, Profesa Dusan Kondic na akaendelea hata
alipoondolewa mwalimu huyo na kuletwa Mseribia mwingine, Kostadin Papic.
Ni
kati ya wachezaji walioiwezesha Taifa Stars kukata tiketi ya kucheza
fainali pekee za michauno ya Ubingwa wa Afrika (CHAN) zinazohusisha
wachezaji wanaocheza ligi za nchini mwao pekee.
Hata
hivyo, Maximo akamtema katika kikosi cha Stars baada ya fainali za CHAN
nchini Ivory Coast mwaka 2009 kutokana na kuwa majeruhi.
Maumivu hayo yalimfanya aachwe na Yanga mwaka 2011 akaenda kumalizia soka yake Simrik SYC ya Nepal.