Mwenyekiti
wa Chadema, Freeman Mbowe amelaani kitendo cha polisi wa Mkoa wa Geita
kumshikilia kwa zaidi ya saa tatu Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa
alipokuwa njiani kwenda kwenye mkutano wa kampeni za uchaguzi mdogo Kata
ya Nkome wilayani Geita juzi.
Hata
hivyo, Jeshi la Polisi limesema halikumkamata mjumbe huyo wa Kamati Kuu
ya Chadema, badala yake lilimwita kituoni kwa ajili ya kuhakikisha
usalama wake na wa wananchi waliokuwa wamemzunguka.
Akizungumza
na waandishi wa habari jijini Mwanza jana, Mbowe alisema huo ni
mwendelezo wa ghiliba, hila na unyanyasaji unaofanywa na Jeshi la Polisi
dhidi ya viongozi wa vyama vya upinzani kwa lengo la kuinufaisha CCM.
Akifungua
kikao cha dharura cha Kamati Kuu ya Chadema, Mbowe alipinga maelezo ya
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Geita, Mponjoli Mwabulambo kuwa
walimshikilia Lowassa kwa usalama wake, akihoji sababu za kuchukua
maelezo yake.
“Tumesikia
maelezo yaliyotolewa na kamanda wa Polisi kuwa Lowassa alishikiliwa kwa
usalama wake. Unayemlinda usalama wake unamwandikisha maelezo?” alihoji Mbowe.
Alisema lengo la polisi, lilikuwa ni kuhakikisha kuwa Lowassa hafiki na kuhutubia mkutano wa kampeni.
Akizungumzia
kuzuiwa kwa shughuli za kisiasa nchini, kiongozi huyo alilitaka jeshi
la polisi kuacha umma uonyeshe mapenzi yao kwa viongozi wanaowapenda.
“Nchi
hii inastahili kuongozwa katika misingi ya sheria badala ya chuki,
ghiliba na ukandamizaji kama tunavyoshuhudia hivi sasa,” alisema.
Alisema
ukimya na upole wa vyama vya siasa kunyamazia ukandamizwaji,
usichukuliwe kuwa ni udhaifu bali ni busara inayolenga kuepusha jamii na
mgawanyiko kiitikadi.
Lowassa
aliyegombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 kwa tiketi ya Chadema
baada ya kujiengua kutoka CCM, alishikiliwa mjini Geita kuanzia saa 9:30
alasiri hadi saa 12:52 jioni baada ya kusimama na kuwasalimia wananchi
waliojitokeza alipokuwa eneo la soko kuu.
==> Msikilize Hapo Chini Akizungumza
==> Msikilize Hapo Chini Akizungumza