WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Bw.
Rashid Taka na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Bw. Raphael Siumbo kufanya
uchunguzi na kuwachukulia hatua watendaji wote watakaobainika kuhusika
katika uuzwaji wa kiwanja cha shule ya msingi Waso.
Ametoa
agizo hilo Alhamisi, Desemba 15, 2016 wakati akihutubia wananchi katika
mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye kata ya Waso Wilaya ya Ngorongoro
akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Arusha.
Waziri
Mkuu alisema Serikali haiwezi kuvumilia kuona watendaji wachache
wasiokuwa waadilifu wanamega kiwanja cha shule na kukiuza kwa maslahi
yao, hivyo aliwataka viongozi hao kufuatilia na kumpa taarifa ya hatua
za kisheria walizochukua kwa wahusika.
“Mkuu
wa wilaya na Mkurugenzi hapa kuna malalamiko ya viwanja fuatilieni
viwanja hivyo vinavyolalamikiwa na wananchi ni viwanja gani je hiyo ya
kwamba mmeuza viwanja vya shule ameuziwa nani,” alisema.
Aidha, Waziri Mkuu amemtaka Bw. Taka ahakikishe Mkuu wa Idara ya
Ardhi,
Maliasili na Mzingira, Bw. Switbeth Byorushengo anatekeleza majukumu
yake ipasavyo. Ametoa agizo hilo baada ya wananchi kudai Ofisa huyo
ameshindwa kufanya kazi na kumuomba Waziri Mkuu aondoke naye.
Alisema
Bw. Byorushengo anatakiwa kuhakikisha halmashauri hiyo inapima viwanja
vya kutosha na kutoa hati kwa wananchi ili waweze kupata maeneo ya
kujenga makazi na shughuli zingine za kijamii.
Katika
hatua nyingine, Waziri Mkuu alimuagiza Mkurugenzi wa halmashauri hiyo
Bw. Byorushengo kuhakikisha halmashauri hiyo inaanza ujenzi wa hospitali
ya wilaya na ifikapo Aprili, 2017 awe amepewa taarifa za ulipofikia
ujenzi huo.Kwa upande wake Mkurugenzi huyo alisema tayari wapo katika
mchakato wa ujenzi wa hospitali ya wilaya ambapo wametenga sh. milioni
800 za kuanzia.
Akizungumzia
kuhusu mgogoro wa ardhi kati ya vijiji vya Tarafa ya Loliondo na
Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Waziri Mkuu alitoa muda wa siku 30 kwa
uongozi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Nchini (TANAPA) wawe
wamekamilisha uhakiki wa mpaka huo.
Naye
Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi ambaye ni Mbunge wa Ngorongoro
Mheshimiwa William Ole Nasha alimuomba Waziri Mkuu kuwasaidia kutatua
mgogoro huo wa ardhi kwa kuwa ni wa muda mrefu na unakwamisha shughuli
za maendeleo.
Awali,
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Bw. Mrisho Gambo alisema Wilaya ya Ngorongoro
inachangamoto nyingi ikiwemo ya ardhi na sasa kuna mgogoro kati ya
Kampuni ya Thomson Safari na wananchi ambao wanadai kuwa ardhi hiyo
ilichukuliwa kinyemela na mwekezaji huyo bila ya wao kushirikishwa.
Alisema
baada ya ziara ya Waziri Mkuu kumalizika mkoani hapa atarudi wilayani
Ngorongoro kwa ajili ya kutatua kero mbalimbali ikiwemo ya ardhi na
matumizi mabaya ya fedha zinazotolewa na wawekezaji ambazo matumizi yake
hayajulikani.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,