WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi aliyekuwa Mwekahazina wa
Halmashauri ya Wilaya ya Longido, Bw. Issai Mbilu ambaye kwa sasa
amehamishiwa Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma na kuagiza arudishwe haraka na
kuja kujibu tuhuma za ubadhilifu sh. milioni 642.4 za miradi
zinazomkabili.
“Tunaendelea
kudhibiti na kuweka nidhamu ndani ya Serikali. Ukiharibu Longido
usitegemee kuhamishiwa wilaya nyingine tunamalizana hapa hapa. Hatuwezi
kuhamisha ugonjwa hapa na kuupeleka wilaya nyingine hivyo Mwekahazina
huyu arudishwe haraka Longido,” amesisitiza.
Waziri
Mkuu ametoa agizo hilo jana Ijumaa, Desemba 16, 2016 wakati akizungumza
na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido kwenye ukumbi wa
Halmashauri hiyo akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Arusha.
Pia
amemuagiza Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Bw. Richard Kwitega
kumuandikia barua Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali
za Mitaa (TAMISEMI) akimuomba amrudishe Mwekahazina huyo katika kituo
chake cha kazi cha zamani ili aweze kujibu tuhuma zinazomkabili.
Amesema
Serikali haitamvumilia mtumishi wa idara yoyote atakayeharibu jambo
halafu kuhamishwa sehemu nyingine, “hivyo naagiza kuanzia sasa
nimemsimamisha kazi Mwekahazina huyu na arudi hapa kujibu kwanini
ameleta hasara ya hizi fedha. Na nyie watumishi wengine hili liwe funzo
kwenu,” amesema.
Amesema
miradi mingi ya maendeleo inakwama kwa sababu ya baadhi ya watumishi
kuweka mbele maslahi binafsi badala ya kuzingatia maadili ya utumishi,
hivyo amewaagiza Wakuu wa Idara wafuatilie kwa makini miradi
inayotekelezwa katika maeneo yao kama inalingana na thamani halisi ya
fedha zilizotolewa.
Akizungumzia
kuhusu kushamiri kwa biashara haramu ya dawa za kulevya wilayani
Longido, Waziri Mkuu amewaagiza wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama
ya wilaya kufanya kufanya msako wa nyumba hadi nyumba na kuwakamata wote
watakaokutwa wanafanya biashara hiyo.
“Wilaya
hii ina sifa mbaya ya kuwa kitovu cha kusafirisha dawa ya kulevya
zikiwemo bangi na mirungi. Hivyo nawaagiza wajumbe wa Kamati ya Ulinzi
na Usalama waendeshe msako kwa kila nyumba na atakayekamatwa achukuliwe
hatua. Dawa za kulevya zinadhohofisha nguvu kazi ya Taifa,”.
“Ukivuta
bangi unapishana na kauli mbiu ya Hapa Kazi Tu kwani unakwenda kulala
jambo ambalo hatuwezi kulikubali. Watakaokutwa wanauza au kununua
mirungi na bangi wakamatwe na kuchukuliwa hatua za kisheria ikiwa pamoja
na kutaifisha magari yanayotumika kubeba bidhaa hiyo haramu,” amesema.
Awali,
Mkuu wa Wilaya hiyo Bw. Daniel Chongolo akisoma Taarifa ya Wilaya
amesema Longido inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kutumika
kama njia kuu ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya bangi na mirungi
kwenda nchi jirani ya Kenya ambako biashara hiyo imehalalishwa.
Changamoto
nyingine ni ukosefu wa hospitali ya wilaya hali inayofanya wananchi
kwenda kutibiwa Kenya, ambapo Waziri Mkuu alisema haiwezekani wakakosa
hospitali ya wilaya hivyo amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo
kuhakikiusha anatenga fedha za ujenzi huo.
Katika
hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Serikali ipo mbioni kujenga kiwanda
cha kuchakata madini ya magadi soda ili yawe na ubora na thamani kubwa.
Ametoa kauli hiyo aliposimamishwa na wananchi katika kijiji cha
Loonolwo kilichopo Kata ya Gelai Merugoi Wilayani Longido akitokea
wilayani Ngorongoro.
Amesema
lengo la kujenga kiwanda hicho ni kuwawezesha wananchi wa wilaya hiyo
hasa akinamama wanaoishi karibu na Ziwa Natron linalotoa magadi hayo
waweze kunufaika na uwepo wa ziwa hilo.
Waziri
Mkuu amesema ujenzi wa kiwanda hicho utawezesha vijana na akinamama hao
wanaouza magadi maeneo ya pembezoni mwa barabara katika ziwa Natron
kupata ajira kwa kuwa kitazalisha ajira zaidi ya 500 katika wilaya hizo
mbili za Longido na Ngorongoro.
Pia
amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Bw. Mrisho Gambo kushirikiana na
wataalam wake kufanya tathimini ya uhaba wa chakula katika wilaya za
Longido na Ngorongoro ili Serikali ijue Mkoa wa Arusha una ukosefu wa
chakula kwa kiasi gani.
"Gambo
fanya tathimini ya hali ya njaa katika wilaya hizi mbili ili tuweze
kuwasaidia wananchi hawa. Hata hivyo nawaomba wananchi mtunze kiasi cha
chakula mlichonacho na marufuku tumia nafaka kwa ajili ya kupika pombe,”
amesema.
Awali,
wananchi hao waliokuwa na mabango mbalimbali walilalamikia kero ya
mipaka ya ardhi kati ya vijiji vya wilaya za Longido na Ngorongoro,
ambapo Waziri Mkuu alimuagiza Afisa Ardhi Mkoa wa Arusha, Bw. Hamdoun
Mansour kwenda katika vijiji hivyo vya mpakani na kukutana na viongozi
wa kimila ili kumaliza mgogoro huo.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,