MKUU wa Mkoa wa Dar es Dalaam,
Paul Makonda jana Desemba 15, 2016 alifanya ziara kwenye Masoko ya
Kariakoo jijini Dar na kufanya mazungumzo na wafanyabiashara na viongozi
mbalimbali wa Shirikia la Masoko hayo.
Akiambatana na Mkurugenzi wa Jiji la Dar
es Salaam, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna
Simon Sirro, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Happy, Mkurugenzi wa
Manispaa ya Ilala na wengine, Makonda amebaini ufujwaji mkubwa wa pesa
za shirika hilo huku hali ikionesha kuwa Shirika la Masoko ya Kariakoo
linajiendesha kwa hasara.
Akijibu maswali ya RC Makonda, Meneja wa
Shirika la Masoko ya Kariakoo amekiri kuwa wanajiendesha kwa kupata
hasara kwani pesa wanayoingiza kama makusanyo ya ushuru yanakuwa ni
kidogo ikilinganishwa na matumizi yao.
Aidha meneja huyo alishindwa kueleza kwa
nini stakabadhi wanaotoa kwa wateja wao hazina Kodi ya Ongezeko la
Thamani (VAT) wakati stakabadhi za michezo ya bahati nasibu ya Betting zina VAT.
Mbali na hiyo Meneja huyo amejitetea
kuwa pesa wanayokusanaya kama shirika wanalipa mishahara ya wafanyakazi
ambapo pia amekiri kuwepo na changamoto nyingi zinazolikabili shirika
hilo ikiwemo miund mbinu chakavu ya soko.
Kwa upande wao wafanya biashara wadogo
wadogo walihoji uhalali wa kupandishiwa ushuru kutoka shilingi 800/=
hadi shilingi 3,000/= huku wakiongezewa rundo la ushuru ikiwemo wa
mezani, ulinzi n.k. ambapo meneja huyo alishindwa kujibu kinaga ubaga.
RC Makonda ameagiza uongozi wa shirika
ufanye kikao na manispaa ya jiji ili kuweka mikakati ya kuboresha soko
hilo pamoja na kuanzisha masoko mengine ambayo yatatokana na soko la
kariakoo.
Viongozi wa Soko la Kariakoo Wanavyofuja Pesa za Mapato