Kwa
muda wa siku tatu sasa Jeshi la Polisi Tanzania linamshikilia
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Jamii Media Limited, Maxence Melo
katika Kituo Kikuu cha Polisi Mkoa wa Dar es Salaam.
Hadi
sasa, si Melo, familia yake au wanasheria wake walioelezwa kosa
linalomfanya ashikiliwe. Wanasheria wa Melo wameweka kambi katika Kituo
Kikuu cha Polisi Dar es Salaam, lakini hakuna majibu ya maana wanayopewa
na wala Melo hafikishwi mahakamani.
Taarifa
wanazotoa askari waliopo kituoni hapo, ambazo si taarifa rasmi, ni
kwamba Melo anashikiliwa kwa nia ya kumtaka awape polisi majina
wanayoyahitaji ya wachangiaji wa masuala mbalimbali katika mtandao wa
Jamii Forums kwa mujibu wa Sheria ya Makosa ya Mtandaoni huku wakidai ni
maelekezo kutoka “juu”.
Siku
ya Jumatano, Desemba 14, 2016 polisi wamefika ofisini na nyumbani kwa
Melo wakapekua sehemu zote. Taarifa kutoka ofisini kwa Melo zinaonyesha
polisi wamechukua nyaraka mbalimbali ikiwamo hati ya kusajili kampuni,
leseni ya biashara na nyingine.
Pia polisi wameondoka na wafanyakazi wawili wa Kampuni ya Jamii Forums kwa mahojiano zaidi.
Taarifa
nyingine zinaonyesha kuwa polisi wanaomshikilia Melo wanajiapiza kuwa
hata kama mawakili wake watakwenda mahakamani hawatamwachia hadi
atekeleze wakitakacho.
Jukwaa
la Wahariri Tanzania (TEF) linafuatilia kwa karibu mwenendo na utendaji
wa Jeshi la Polisi juu ya suala la uhuru wa kujieleza na kutoa maoni
unaotolewa na Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
(1977).
Katika
siku za karibuni, TEF na Watanzania kwa ujumla wanashuhudia ukiukwaji
mkubwa wa haki za binadamu unaofanywa na Jeshi la Polisi linaloelekea
kuacha kuheshimu misingi ya utawala wa Sheria na Katiba ya Tanzania.
Melo
kama mtuhumiwa anayo haki ya kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma katika
muda usiozidi saa 24. Kitendo cha polisi kumshikilia kwa siku tatu,
ambapo hatujui kama anateswa au la, ni uvunjaji mkubwa wa haki za
binadamu.
Tamko
la Haki za Binadamu la Mwaka 1948 linavitaka vyombo vya dola kuheshimu
utawala wa sheria ambao pamoja na mambo mengine msingi wake ni kuheshimu
mgawanyo wa madaraka (separation of power). Kitendo cha Polisi kuanza
kuchukua sheria mkononi kwa kukamatakamata watu, kuwatisha waandishi wa
habari na watetezi wa haki za binadamu hakikubaliki.
TEF
inalitaka Jeshi la Polisi kumwachia mara moja Melo bila masharti au
kumfikisha mahakamani na kumfungulia mashitaka kwa mujibu wa sheria
ikiwa ana kosa.
Tunamwomba
Rais John Magufuli aingilie kati mzozo huu na kuwafahamisha polisi kuwa
wanayoyatenda wanapalilia mbegu ya chuki katika nchi jambo ambalo si
jema waliache mara moja.
TEF
inaungana na Watanzania kulaani kitendo cha polisi kumkamata Melo kwa
kutumia sheria mbaya isiyokubalika ya Makosa ya Mtandaoni.
TEF
inatetea haki ya uhuru wa kutoa mawazo na kukataa ukandamizaji huu wa
polisi wanaodai wana maelekezo kutoka juu chini ya uongozi wa Serikali
ya Awamu ya Tano. Mungu ibariki Tanzania.
Theophil Makunga,
Mwenyekiti,
Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF)
Dar es Salaam, Desemba 15, 2016