Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameweka jiwe la msingi katika mradi mkubwa wa maji kwenye mji Nansio katika kisiwa cha Ukerewe mkoani Mwanza mradi ambao utahudumia wananchi elfu 61.
Makamu wa Rais ambaye jana alisafiri kwa takribani masaa Matatu na meli ya MV Nyehunge II katika Ziwa Victoria kwenda kisiwa hicho kwa mara ya kwanza tangu ashike wadhifa huo,aliwahimiza
wananchi hao wautunze mradi huo ambao utasaidia kwa kiasi kikubwa
kuondoa tatizo na uhaba wa maji safi na salama katika kisiwa hicho.
Mradi
huo ambao unaojumuisha kazi za uboreshaji wa huduma ya majisafi na
usafi wa mazingira unatekelezwa chini ya umefadhili wa Benki ya
Maendeleo ya Afrika (AfDB) na serikali ya Tanzania katika miji ya
Sengerema,Geita na Nansio – Ukerewe kwa gharama ya Dola za Kimarekani
milioni 30.4 ambapo serikali ya Tanzania imechangia mradi huo Dola za
Kimarekani milioni nne.
Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan aliwaahidi wananchi kuwa serikali ya awamu ya Tano inamikakati
mizuri inayolenga kuondoa tatizo la maji kote nchini ili kusaidia
wananchi hao hasa wanawake kutumia muda mwingi kufanya kazi za maendeleo
kuliko kutafuta maji.
Akihutubia
mamia ya wananchi wa kisiwa cha ukerewe kwenye kijiji cha Kagunguli
mkoani Mwanza mara baada ya kuweka mawe ya msingi katika miradi miwili
ukiwemo mradi wa maji na ujenzi wa chumba cha upasuaji katika kituo cha
afya cha Kagunguli, Makamu wa Rais aliwapa
pole wananchi wa kisiwa hicho baada ya kukumbwa na tufani ya kimbunga
cha upepo iliyotokea tarehe 04 Novemba 2016 na kusababisha uharibifu
mkubwa ikiwemo nyumba za watu kubomoka.