Wakati
wadau wa umeme wa jijini Dar es salaam wakisubiri wiki ijayo kutoa
maoni kuhusu pendekezo la Tanesco kuongeza bei ya umeme kwa asilimia
18.19, wenzao katika kanda nne wamepiga hatua hiyo.
Msimamo
huo umetolea katika mikoa ya Arusha, Mwanza, Dodoma na Mbeya ambako
vikao vya kukusanya maoni ya wadau vimefanyika chini ya Mamlaka ya
Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati (Ewura).
Jijini Mwanza.
Maofisa
wa Tanesco, juzi walijikuta kwenye wakati mgumu kujibu hoja za wadau wa
Kanda ya Ziwa kuhusu kutaka kupandisha bei, miezi michache tangu
ipunguze kwa asilimia 1.1.
Pia,
wadau waliwabana maofisa hao kueleza ni kwa nini shirika hilo
halikusanyi madeni sugu kutoka serikalini na taasisi za umma, badala
yake inawabebesha mzigo watumiaji wa chini ambao hulipia huduma kabla.
Mwenyekiti
wa Kamati ya Walaji wa Bidhaa zinazodhibitiwa na Ewura Mkoa wa Mwanza,
Jerry Mwasa alisema Tanesco imekosa ubunifu kiutendaji licha ya taifa
kujaliwa vyanzo vingi vya umeme ikiwamo gesi asilia, makaa ya mawe,
upepo na joto ardhi.
“Ni
aibu maofisa wa Tanesco kuja hapa kudai eti bei za umeme Tanzania ni
nafuu kulinganisha na Kenya, Uganda na Rwanda ambao hawana gesi wala
makaa ya mawe kama Tanzania,” alisema Mwasa.
Akiwasilisha
maoni ya Baraza la Ushauri la Walaji (Ewura CCC), Kaimu Mwenyekiti wa
baraza hilo, Thomas Mnunguli alihoji ukinyonga wa Tanesco ambayo Machi 4
iliahidi kupunguza bei ya umeme kwa asilimia 7.9 ifikapo mwakani,
lakini ghafla imebadilika na kutaka kuipandisha kwa asilimia 18.19.
“Kwa
maoni yetu, Ewura ikatae maombi haya, badala yake Tanesco waagizwe
kutekeleza agizo la kuwasilisha mpango mkakati wa kuboresha huduma,
kupunguza bei na kukusanya madeni kutoka kwa wadaiwa sugu ikiwamo
serikali na taasisi za umma,” alisema Mnunguli.
Kaimu
Mwenyekiti wa Baraza la Ushauri la Serikali (GCC), Amani Mafura
alishauri upandishaji wa bei ya umeme ufanyike kwa awamu ili isiathiri
mpango wa Serikali wa kujenga “Tanzania ya viwanda” wala juhudi za
wananchi kujikwamua kiuchumi.
Mmoja wa wadau, Frank Zekenuka alisema:
“Wakati wateja tunalipia nguzo ambayo hata hivyo inasalia kuwa mali ya
Tanesco, bado shirika hili linadai kuelemewa gharama za usambazaji. Hiki
ni kiini macho cha kutulainisha tukubali ombi la kupandisha bei.”
Katika
kikao cha Kanda ya Kati kilichofanyika Dodoma, wadau walisema kiasi
kinachotakiwa kupandishwa ni kikubwa na mwananchi wa kawaida hataweza
kukimudu.
Mwakilishi
wa Ewura-CCC, Erasto Kishe alisema badala ya shirika hilo kupandisha
bei ya umeme, linatakiwa kushusha kwa kuwa shughuli zote za maendeleo
zinahitaji nishati hiyo hivyo hatua hiyo itapandisha gharama za maisha.
“Baraza
linashauri Tanesco ianze kuwakatia umeme wadaiwa wake sugu ili
kulazimisha kulipa madeni yao pamoja na riba kama zilivyo kanuni zake.
Mjumbe
wa GCC, Ezamo Mponde aliitaka Ewura iitake Tanesco kutoa maelezo ya
kina kwa nini inataka kupandisha bei kwa kipindi cha mwaka mmoja tu
tofauti na utaratibu uliopo wa kufanya hivyo kwa kipindi cha miaka
mitatu.
“Ukipandisha
gharama za umeme ni wazi kila kitu kitapanda bei na kama sababu ni
kupanda kwa gharama za uzalishaji pamoja na madeni mliyonayo ni bora
kama mngeirudisha ile asilimia 1.1 ambayo mliipunguza Aprili kuliko
kuongeza bei kwa asilimia 18.19 baada ya miezi saba tu,” alisema Mponde.
Huko
Mbeya, Ewura CCC imeitaka Tanesco kuweka mipango madhubuti ya kukusanya
mapato kutoka kwa wadaiwa sugu walipe pamoja na riba badala ya kutaka
kuongeza bei.
Mjumbe
wa baraza hilo, Julius Mwambeso alisema Tanesco inaweza kupata fedha
nyingi kama itakuwa makini kukusanya madeni ya wateja 4,036 wanaodaiwa
Sh3.2 bilioni na kubana matumizi ya vikao vya bodi ambavyo vinafanyika
mara 49.
Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Paul Ntinika alisema Serikali inatoa mchango wake kwa Tanesco ili iweze kuwapunguzia makali wananchi.
Alisema
hategemei kuona ongezeko lolote la bei ya umeme kutokana na ukweli
kwamba Serikali ingependa wananchi wapate unafuu zaidi.
Maoni ya Tanesco
Naibu
Mkurugenzi Mkuu (Usafirishaji Umeme) wa Tanesco, Kahitwa Bishaija
alisema shirika hilo limelazimika kuwasilisha ombi la kupandisha bei ili
kumudu gharama za uzalishaji, usafirishaji, usambazaji na kuboresha
huduma kwa wateja.
Alisema
licha ya uzalishaji kwa kutumia gesi asilia kuongezeka kutoka asilimia
47 mwaka 2015 hadi asilimia 58 mwaka huu, huku matumizi ya mafuta mazito
kuzalisha umeme yakibakia asilimia tano pekee kulinganisha na asilimia
19 ya zamani, bado shirika hilo linakabiliwa na hali ngumu kiuendeshaji
kutokana na madeni.
Alisema
deni la Tanesco limeongezeka kutoka Sh699.57 bilioni Desemba mwaka jana
hadi Sh794.48 Septemba na kwamba licha ya kuongeza mapato hadi kufikia
Sh1,042.5 bilioni kulinganisha na Sh995.3 bilioni za mwaka jana,
inalazimika kutumia wastani ya asilimia 13 ya mapato yake kwa mwezi
kununulia mafuta ya kuzalisha umeme.
Bishaija
aliwaeleza wadau kuwa ukokotoaji wa bei mpya inayoombwa umezingatia
gharama ya ufuaji umeme, usafirishaji, usambazaji, uchakavu na
uendeshaji.
Mhandisi
kutoka Tanesco, Sophia Mgonja alisema ongezeko hilo la bei linatokana
na ukame ulioikumba nchi kutokana na mvua kutonyesha kwa kiwango
kinachotakiwa na kwamba kina cha maji katika Bwawa la Mtera ni kidogo
hivyo wasipofanya juhudi za kutafuta vyanzo vingine vya kuzalishia
umeme, kutakuwa na mgawo.
“Pia
kama mnavyofahamu kuwa mamlaka ya utabiri wa hali ya hewa umeshatabiri
kuwa mwaka huu hakutakuwa na mvua za kutosha hivyo kama tusipofanya
juhudi za kutafuta vyanzo vingine vya kuzalishia umeme tunaweza kukwama
huko mbeleni,” alisema Mgonja.