Mahakama moja mjini Tehran, Iran imemhukumu aliyekua mkuu wa mashtaka ya umma viboko 135 kwa makosa ya ufisadi.
Vyombo vya habari vinasema Saeed Mortazavi alipatikana na hatia ya ubadhirifu wa mali ya umma. Makosa hayo yalitokea wakati akiwa mkuu wa idara ya huduma ya jamii miaka ya 2012 na 2013.
Afisa huyo wa zamani aliwahi kuwekewa vikwao na Marekani kwa tuhuma za ukiukaji wa haki za binadamu. Runinga ya taifa imesema wakuu wa mashtaka wamelalamikia hukumu hiyo kuwa na chini sana na kwamba wanapanga kuwasilisha lalama.
Saeed Mortazavi alikua mshirika wa karibu wa Rais wa zamani Mahmoud Ahmadinejad na amekosolewa vikali sana na mirengo inayounga mageuzi na makundi ya haki za binadamu.
Alijulikana zaidi miaka ya 2000 ambapo alichangia pakubwa kufunga magazeti yaliyotetea mageuzi na pia kuwafungia gerezani waandishi habari.Pia alihusishwa na kesi ya Zahra Kazemi mpiga picha mwenye uraia wa Canada na Iran ambae alikufa baada ya kukamatwa.
Masaibu yake yalianza pale serikali ilipozima maandamano kulalamikia matokeo ya kura ambapo Bwana Ahmadinejad alitangazwa mshindi mwaka wa 2009. Bunge lilimlaumu kwa kusababisha vifo vya waandamanaji watatu waliokufia gerezani.
Waandamanaji hao walifariki dunia kutokana na majeraha waliopata ndani ya gereza. Kiongozi Mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei aliitikia kilio cha umma na kufunga gereza hilo. Mortazavi aliteuliwa baadae kusimamia idaya ya huduma ya jamii ambapo ilidaiwa kutokea visa vya ufisiadi.
Bunge lilishinikiza kuondolewa kwake, lakini baadae Ahmadinejad akamteua kama kaimu mkuu wa idara hiyo.Mwaka wa 2014, Mortazavi aliwekewa marufuku ya miaka mitano dhidi ya kusimamia afisi ya umma.
Hii ni baada ya Mahakama ya Juu kumpata na hatia ya kuamrisha mateso dhidi ya waandamanaji watatu waliofariki dunia wakiwa ndani ya jela.Iran imeendelea kutumia adhabu zinazokosolewa na jamii ya kimataifa. Baadhi ni pamoja na kung'oa macho ya wahalifu, kukata mikono na miguu na kuwafanya wahalifu kuwa viziwi.