Kamanda
wa Polisi mkoa wa Dar es salaam Simon Sirro, amesema kama Mkuu wa mkoa
wa Dar es Salaam Paul Makonda, ana wasiwasi na Jeshi la Polisi katika
operesheni ya kutokomeza matumizi ya Shisha, achukue hatua zaidi kwa
sababu yeye ni kiongozi wao na ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na
Usalama Mkoani Dar es salaam.
Akiongea
kupitia kipindi cha Sun Rise cha Times Fm leo asubuhi, Sirro amedai wao
kama jeshi la Polisi wanafanya kazi kwa mujibu wa Sheria na Operesheni
ya kutokomeza Shisha jijini inaendelea kama kawaida kilicho baki ni
Mwanasheria mkuu wa Serikali kuandaa mashtaka kwa Watuhumiwa.
“Watu
wamekamatwa ni wengi, kimsingi kazi inafanyika, sasa huo ni wasi wasi
kama wasi wasi basi unabaki kuwa wasi wasi, kikubwa niseme tunafanya
kazi kwa mujibu wa sheria na kanuni, yeye ni mwenyekiti wangu wa kamati
ya ulinzi na usalama kwa hiyo ninaamini kama ana wasiwasi na chombo
chake najua atakuja kutuita na kutuambia nini cha kufanya.
“Lakini
kama ana wasi wasi Zaidi yeye ni kiongozi wetu atajua atachukua hatua
gani dhidi ya sisi, kwa hiyo namuachia mkuu wangu wa kazi yeye ndio
atajua nini cha kufanya”
Akitolea
ufafanuzi kama alipatiwa taarifa juu ya watu 10 waliotaka kumpa
‘Mlungula’ Mkuu wa Mkoa ili kumziba ‘Mdomo’ kukemea matumizi ya kilevi
cha Shisha, Kamanda Siro alisema hawezi kulisemea lolote swala hilo na
amemtaka Mtangazaji wa Sun Rise Stanslaus Lambat amuulize Mh Makonda
taarifa aliipeleka wapi na si yeye.