Sheria ya Tawala za Mikoa ya mwaka 1997, kifungu cha 15 (1) inawapa mamlaka wakuu wa mikoa na wilaya kutoa amri ya mtu kukamatwa na kuwekwa ndani kwa saa 48 pale anapobaini kwamba mhusika ametenda kosa fulani.
Wakuu wa wilaya sasa wanatumia mamlaka hayo pale watendaji wao wanaposhindwa kutimiza maagizo yao. Suala la watendaji kuwekwa ndani limeshuhudiwa katika wilaya za Sengerema, Arumeru, Rorya na Newala.
Oktoba 13 mwaka huu, Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Emmanuel Kipole alimsweka ndani kwa saa 12 kaimu mkurugenzi wa wilaya hiyo, Oscar Kapinga na kaimu mhasibu wa halmashauri hiyo, Paul Sweya kwa kushindwa kutekeleza agizo la mkuu huyo la kutafuta fedha kwa ajili ya kuwalipa wanaofanya usafi katika mji wa Sengerema.
Inaelezwa kuwa watu hao wanaofanya usafi hawajalipwa fedha zao kwa zaidi ya miezi sita, jambo lililomsukuma Kipole kuagiza walipwe.
Tukio jingine ni lile la Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Alexander Mnyeti kuwaweka ndani madiwani wanne wa Chadema kwa madai kwamba wamekuwa wakimkwamisha kutekeleza kazi zake.
Miongoni mwa waliowekwa ndani ni mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo, Noah Lembrise ambaye alilala katika Kituo cha Polisi cha Usa River. Wengine ni Happy Gadiel, Nuru Ndosi na Winfrida Lukumay.
“Hawa (madiwani) wamekuwa wakivuruga ziara zangu kwa kupita kwa wananchi na kupotosha dhima ya Serikali kuhusu maendeleo.”
Huko Newala, Mkuu wa Wilaya, Aziza Mangosongo alimlaza katika Polisi kaimu meneja wa Mamlaka ya Maji Mradi wa Makondeko, Athumani Semkondo na fundi Mohamed Salum kwa saa 48 kwa kuvikosesha maji vijiji 14 vyenye wakazi 60,000.
Mangosongo alisema kulifanyika hujuma ya kuziba bomba ili maji yasipatikane katika vijiji hivyo lakini kaimu mkurugenzi huyo alishindwa kufuatilia taarifa aliyopewa kwamba vijiji hivyo havipati maji ili achukue hatua.
“Kama mkurugenzi alikuwa na taarifa na hakuchukua hatua, kuna nini kimejificha hapo? Lazima nitahisi kuna jambo ndiyo maana nikaamua akalale rumande kwa saa 48 kwa sababu nina mamlaka kisheria. Akae humo ndani kwanza ajitafakari,” alisema Mangosongo.
Hali kama hiyo ilitokea pia katika Wilaya ya Rorya baada ya mkuu wa wilaya hiyo, Simon Chacha kuwaweka ndani watu 10 akiwamo Diwani wa Kigunga (Chadema), Vitalis Joseph baada ya kutokea mgogoro kati ya vijiji viwili na kusababisha mazao kufyekwa.
Diwani huyo alifika eneo la tukio na kukuta mazao yamefyekwa, hata hivyo, Chacha aliagiza akamatwe na kuwekwa ndani pamoja na watu wengine kwa kuhusishwa na uharibifu huo.
“Tumewachukua baadhi ya watu ili kuisaidia Serikali kupata uhalisia wa tukio hili, na ninawaambia wananchi wa Rorya kuwa Serikali hii ya awamu ya tano haitaki mzaha na yeyote anayejitokeza kufanya vitendo viovu tutamshughulikia,” alisema Chacha.
Maoni ya wadau
Wadau mbalimbali wamepinga hatua ya wakuu wa wilaya kuwaweka ndani watendaji wa halmashauri wakisema wanafanya hivyo kwa lengo la kuwakomoa.
Profesa wa Chuo Kikuu cha Ruaha (Rucu), Gaudence Mpangala amesema amri hizo zimekuwa zikitolewa katika maeneo ambayo upinzani unaongoza, jambo analolitafsiri kama ni kuwakomoa wapinzani.
Alisema sheria hiyo inatumika kukandamiza demokrasia kinyume na malengo ya kuanzishwa kwake. Alisema wakuu wa wilaya wanatakiwa kutumia sheria inayowapa mamlaka hayo kwa wahalifu wa makosa ya jinai na wahujumu uchumi.
“Madiwani na wakurugenzi ni watendaji tu, kuwaweka ndani kwa kushindwa kutekeleza maagizo ya mkuu wa wilaya ni kuwaonea. Sheria hiyo ya saa 48 itumike kwa wahalifu na wanaohujumu uchumi,” alisema.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Benson Bana alisema sheria inayotumika bado ina sura ya kikoloni kwa sababu haiendani na taratibu za menejimenti ya watumishi.
Alisema kumweka mtumishi ndani siyo njia nzuri ya kumwajibisha kwa sababu uongozi wa sasa unafuata mfumo wa kufanya kazi kwa pamoja.
“Unapomweka mtu ndani tayari umemhukumu na mara nyingi amri hiyo inatolewa na wakuu wa wilaya ili kuonyesha kwamba wana uwezo wa kufanya jambo,” alisema.
Katibu Mkuu wa CCK, Renatus Muabhi alisema wakuu hao wanataka kujijengea sifa kwa Rais wakidhani kwamba kuwaweka watu ndani ndiyo uwajibikaji.