CHAMA
Cha Mapinduzi (CCM), kimeitaka Serikali kuhakiki akaunti na mali za
Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT) na wenzake waliokuwa katika
kamati za fedha za Bunge, ili kubaini kama zinalingana na kipato
walichokuwa wakipata.
Msemaji
wa chama hicho, Christopher Ole Sendeka, amesema hayo jana
alipozungumza na waandishi wa habari, akimuhusisha Kiongozi huyo Mkuu wa
ACT na tuhuma za ufisadi wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), alipokuwa
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC).
”Nilikuwa
najiuliza hivi chuki ya Zitto kwa Serikali ya Awamu ya Tano,
inayopambana na mafisadi imetoka wapi wakati yeye alikuwa anasimamia
mashirika hayo.
“Miongoni
mwa taasisi hizo alizokuwa akisimamia na baadhi ya marafiki zake ndiyo
hao walionunua hekari moja kwa Sh milioni 800, wakati ilikuwa ikiuzwa
kwa Sh milioni 25 na walikuwa wamejificha kwa maslahi binafsi,” alisema katika ofisi ndogo za Makao Makuu, Lumumba Dar es Salaam.
NSSF
ndiyo iliyonunua hekari 20,000 Kigamboni jijini Dar es Salaam kwa Sh
milioni 800 kwa kila hekari, badala ya Sh milioni 25 na kujikuta katika
hatari ya kupoteza Sh bilioni 270, katika mradi wa ujenzi wa mji wa
kisasa wa Dege Eco Village.
Kutokana
na tuhuma hizo za NSSF zilizoibuka upya katika kamati ya PAC wiki hii,
Sendeka alisema ni vema Serikali ikague kuona kama akaunti za viongozi
wa zamani wa kamati hizo, maisha yao na mali walizonazo, zinafanana na
mapato halali waliyokuwa wakilipwa.
Alisema
alikuwa anaangalia msukumo wa ghafla na mapenzi ya akina Zitto
waliyokuwa wanayapata kwa nchi, kumbe ilikuwa ni kichaka cha kuficha
baadhi ya maswahiba zao wasichukuliwe hatua.
Aliwahakikishia
wananchi kuwa Serikali ya Rais Magufuli haina nia ya kurudi nyuma
katika jambo lolote na kuwa itasonga mbele huku akiamini kuwa Serikali
iliyochaguliwa na watu haiwezi kufa.
“Tunahakika
Serikali ya Magufuli iliyopata ridhaa ya kutumikia watu, haitafutika
kwa kelele za mlango wa baadhi ya makuwadi na watu waliolipwa kuchafua
taswira ya Tanzania,” alisema.
Aliongeza
kuwa Serikali hiyo itaendelea kushughulikia wakwepa kodi pamoja na
kuchunguza mambo aliyoanzisha Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipokuwa
bandarini.
Kauli ya Zitto
Akizungumzia tuhuma hizo, Zitto Kabwe alisema hana muda wa kujibu alichoita kuwa ni porojo na vioja vya Sendeka.
Alifafanua
kuwa CCM ni chama dola na kuna taasisi nyingi za uchunguzi za Serikali,
ikiwemo Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) na Mkurugenzi
wa Mashitaka ya Jinai (DPP) na kushangaa kwa nini vyombo hivyo havisemi,
aseme Sendeka?