test

Jumapili, 18 Septemba 2016

Afya za Madereva Waliotekwa nyara DRC


MADEREVA 13 wa malori raia wa Tanzania na Kenya waliotekwa na waasi wa Maimai nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), kabla ya kuokolewa na majeshi ya serikali, wamewasili katika mji wa Kindu na kufanyiwa uchunguzi wa afya zao.
Waziri wa Mambo ya Ndani anayeshughulikia pia Ulinzi katika mkoa wa Maniema nchini DRC, Saleh Bonne Avanture, alithibitisha madereva hao kuwasili katika mji huo wakiwa salama juzi jioni.

Alisema mara baada ya kuwasili katika mji huo, madereva hao walianza kufanyiwa uchunguzi wa afya ili kuona kama walikuwa wameathiriwa na jambo lolote kutokana na tukio la kutekwa nyara kwao na waasi hao.
Alisema katika uchunguzi huo, madereva hao walibainika kutopata madhara yoyote na kueleza kuwa hatua inayofuata ni kuwatafutia vitambulisho vya Uhamiaji ili kuwasafirisha kurejea nchini Tanzania na Kenya.
Utekaji huo ulifanyika katika eneo la Namoyo, Jimbo la Kivu Kusini, Jumatano jioni na kitendo cha kuwaokoa kilitokana na juhudi za majeshi ya serikali ya DRC, ambayo yalisema yalifanikiwa kuwakomboa bila kutoa gharama zozote.
Madereva hao waliokolewa mafichoni wakiwa wanashikiliwa mateka wakiwa na raia wengine 15 wa DRC ambao nao walikombolewa na kurejea makwao.
Waziri huyo alithibitisha kuwa kundi la waasi wa Maimai ndiyo lililohusika na utekaji nyara huo likitumia mwanya wa kuwepo kwa vurugu katika maeneo hayo ya Kivu.
Alisema jeshi litawasaka waasi hao katika mapori wanakojificha huku akiwaasa wafanyabiashara kuendelea na biashara zao kama kawaida na kwamba kilichotokea ni sawa na ajali.
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mindi Kasiga alipohojiwa ili kufahamu siku madereva hao watakapowasili nchini, alisema bado haijajulikana.
Pamoja na kuwateka nyara madereva hao, waasi hao pia waliyachoma moto malori 10, manane yakiwa yanamilikiwa na mfanyabiashara wa Tanzania Azim Dewji, na mawili ni ya mfanyabiashara kutoka nchini Kenya.
Watekaji hao wa kikundi cha waasi cha Maimai walitaka kulipwa dola za Kimarekani 4,000 (Sh mil 8.8) kwa kila mtu ili kuwaachia huru. Tukio hilo ni la pili kutokea katika miaka ya karibuni ambapo mwaka jana Mashehe kutoka nchini walitekwa nchini DRC lakini kwa ushirikiano wa serikali hizo mbili waliachiwa huru na kurejea nyumbani wakiwa salama.

Install Application ya JUNGUKUULEO Uweze Pata Habari Kirahisi Zaidi

xxxxxxxxxxxxx