WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali haitasita kuwaondoa katika
nyadhifa zao Wakurugenzi wote watakaoshiriki katika kutoa taarifa za
uongo kuhusu miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo
yao.
“Serikali
inatoa fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo ambapo kuna
baadhi ya viongozi wamekuwa wakiandika taarifa za uongo kuwa mradi
umekamilika wakati haujajengwa, hivyo wakurugenzi watakaoshiriki kutoa
taarifa zisizokuwa sahihi wataondolewa,” alisema.
Waziri
Mkuu ameyasema hayo jana jioni (Jumapili, Julai 31, 2016) wakati
akipokea taarifa ya mkoa wa Morogoro mara baada ya kuwasili mkoani hapa
kwa ziara ya kikazi ya siku tatu.
Alisema
alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa wakurugenzi katika halmashauri zote
nchini kuhakikisha wanatembelea miradi yote inayojengwa katika maeneo
yao ili kufanya ukaguzi na kujiridhisha kama thamani yake inalingana na
kiasi cha fedha kilichotolewa.
Katika
hatua nyingine Waziri Mkuu amesema Serikali aihitaji Halmashauri kutoa
ajira za mikataba kwenye kada zilizopo katika muundo wa ajira hivyo
ameziagiza halmashauri zote nchini kufanya mapitio ya watumishi wa
mikataba.
“Tumeruhusu
kuajiri kwa mikataba walimu wa masomo ya sayansi kwa kipindi cha miaka
miwili tena kwa waliostaafu. Kuna kada zilizoko katika muundo wa ajira
hizo hatuhitaji watumishi wa mikataba wakiwemo madereva msiwatumikishe
kwa mikataba watakosa stahili zao,” alisema.
Akizungumzia
suala la watumishi hewa mkoani Morogoro Waziri Mkuu alisema ni vema
wakaendelea kufanya uchunguzi na ifikapo mwisho wa mwezi huu wawe
wamekamilisha taarifa na kuanza kuchukua hatua kwa waliohusika kwa
waliohusika.
Kwa
upande wake mkuu wa mkoa wa Morogoro Dk. Stephen Kebwe katika taarifa
yake aliyoiwasilisha kwa Waziri Mkuu alisema mkoa unaendelea kutekeleza
agizo la Rais Dk. John Magufuli la kuzitaka taasisi zote za Serikali
kufanya uhakiki wa mishahara hewa na malipo batili ya watumishi.
Alisema
mkoa umebaini watumishi hewa 315 ambao wameisababishia Serikali hasara
ya sh. bilioni 2.132 ambapo timu ya uhakiki bado inaendelea na zoezi
hilo na taarifa kamili itatolewa mara kazi hiyo itakapo kamilika.