Watu 14 wamefariki dunia katika wilaya za Chemba mkoani Dodoma na Kiteto mkoani Manyara kutokana na ugonjwa unaojulikana kitaalamu kama ‘Aflatoxicosis’ unaosababishwa na sumu kuvu (Aflatoxins) kwenye nafaka iliyoharibika.
Hayo
yamesema na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto, Ummy Mwalimu wakati akitoa taarifa kwa waandishi wa habari juu
ya magonjwa ya milipuko na magonjwa mengine leo jijini Dar es Salaam....
“Ugonjwa
uliosababishwa na sumu kuvu (Aflatoxins) uliripotiwa kwa mara ya kwanza
tarehe 13 Juni, 2016 katika wilaya za Chemba mkoani Dodoma na baadaye
mkoani Manyara katika wilaya ya Kiteteo” alisema Waziri Ummy na kuongeza kuwa:
“Wagonjwa
walikuwa na dalili za kuumwa tumbo, kuharisha, kutapika, tumbo kuvimba
na kuwa manjano sehemu mbalimbali za mwili ambayo inaashiria kuathirika
kwa ini”
Alisema
mbali na vifo hivyo, hadi kufikia Julai 31 mwaka huu wagonjwa 54
waliripotiwa kuugua ugonjwa hu huku wagonjwa wanne wakilazwa kutokana na
kuugua.
“Hadi kufikia tarehe 31, July
2016 kulikuwa na wagonjwa 54 na watu 14 walipoteza maisha kutokana na
ugonjwa huo.Aidha katika wiki iliyopita aliripotiwa mgonjwa mmoja mpya
kutoka wilaya ya Kondoa” alisema Waziri Ummy na kufafanua kuwa:
“Jumla
ya wagonjwa waliolazwa wodini ni wanne kati yao mmoja yupo Hospitali ya
Rufaa ya Dodoma na watatu wapo katika Hospitali ya Kondoa”
Waziri
Ummy alitaja wilaya zilizoripoti wagonjwa hao na idadi ya wagonjwa kuwa
ni wilaya ya Chemba wagonjwa 38, Kondoa wagonjwa tisa , Kiteto wagonjwa
watatu, Chamwino wagonjwa wawili na Dodoma Manispaa mgonjwa mmoja.
“Vijiji
vilivyoathirika zaidi na ugonjwa huo ni kutoka wilaya ya Chemba ambavyo
ni Kinkima, Itolwa, Mwailanje na katika wilaya ya Kondoa ni kijijini
cha Ubembeni” alisema Waziri Ummy.
Hivyo,
aliitoa hofu familia iliyopoteza watu wanne katika kijiji cha
Mwaikuzabe na kusema vifo hivyo havihusiani na uchawi au kuwekewa sumu
bali ni chakula cha siku ile kilithibitika kwamba kilikuwa na sumukuvu.
Kufuatia
athari hizo Serikali itafanya uchunguzi wa kina katika wilaya kumi za
Chemba, Kondoa, Chamwino na Kiteto na wilaya nyingine za mikoa ya
Sindida, Dodoma na Manyara zinazopakana na wilaya hizo.
Alisema
uchunguzi huo unalenga kubaini hali ya usalama wa vyakula vinavyotumiwa
na jamii ili kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo na kuwaathiri wananchi wengi
zaidi wanaoishi katika wilaya hizo.
Kwa
upande wake Mkurugenzi wa Taifa wa Afya wa Wizara hiyo Dkt. Fausta
Mosha alisema wizara imeandaa vipepereshi vyenye maelekezo yanayotoa
elimu juu ya kijikinga kwa kuandaa chakula kuanzia hatua ya uvunaji
shambani hadi wakati wa kula.
Naye
Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Otilia Gowelle alisema njia bora ya
kupambana na ugonjwa huo ni kuukinga kwa kuhakikisha sumu kuvu
haizalishwi kutoka kwenye nafaka.
Akifafanua
kuhusu udhibiti, Waziri Ummy alisema wanashirikiana na Wizara ya Kilimo
Mifugo na Uvuvi kutoa elimu kwa wananchi juu ya njia sahihi ya uhifadhi
na uandaaji wa chakula utakaosaidia kupunguza kiasi cha sumukuvu kwa
nafaka ambazo hazijaharibika sana.
“Njia
hizi ni pamoja na kuhifadhi nafaka zilizokauka vizuri na kuchambua
nafaka zilizoharibika (zilizooza, kuvunjika, zilizobadilika rangi),
kukoboa mahindi kabla ya kusaga au kuacha kutumia nafaka zitakazoonekana
kuharibika rangi” alisema.
Waziri
Ummy alisisitiza Serikali kuendelea kuimarisha mikakati ya kitaifa ya
kupunguza uchafuzi wa sumukuvu katika vyakula, ikiwa ni pamoja na
kujenga uwezo wa kupima sumukuvu katika damu na choo kidogo miongoni mwa
taasisi za ndani ya nchi.
Inaelezwa
kuwa ugojwa wa‘Aflatoxicosis’unaosababishwa na sumu kuvu (Aflatoxins)
kwenye nafaka uliwahi kutokea nchini Kenya mwaka 2004 na kusababisha
vifo vya zaida ya watu 100 huku wengine 200 waliathirika.