CHAMA
cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Pwani kimeanza kugawa
vifaa zikiwemo bendera kwa ajili maandalazi ya Umoja wa Kupinga Udikteta
( Ukuta) ambayo yanatarajia kufanyika Septemba mosi mwaka huu.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Katibu wa Kanda ya
Pwani wa Chadema, Casimir Mabina, alisema kuwa bendera hizo zitaanza
kupeperushwa kuanzia kesho kutwa kwa ajili ya kuunga mkono azimio la
Kamati Kuu ya kufanyika oparesheni Ukuta.
Alisema
oparesheni Ukuta ni lazima ifanyike nchi nzima na kwamba hawako tayari
kuona ukandamizaji wa demokrasia unaoendelea kufanywa na serikali ya
awamu ya tano ambayo imeonyesha viashiria vya utawala wa kidikteta.
Alisema
Rais John Magufuli, anajaribu kuua demokrasia ya vyama vingi kwa
kukataza na kuzuia mikutano ya kisiasa ya vyama vya upinzani huku CCM
ikiendelea na mikutano yake kama kawaida.
“Tumeona
jinsi Rais alivyopiga marufuku wapinzani kukutana kwenye mikutano ya
hadhara huku akiwatishia kuwa wakikaidi atawashughulikia na kweli
amewaamuru polisi watekeleze amri hiyo ya kuwakamata viongozi wa Chadema
na kuwafungulia mashtaka,” alisema
Aliongezea
kuwa mbaya zaidi Jeshi la Polisi linazuia hata mikutano ya ndani ya
vyama vya upinzani na makongamano na hata mahafali ya wanafunzi wenye
itikadi za upinzani licha ya kutambua kuwa mikutano ya ndani haiwezi
kuleta uvunjifu wa amani kwa walio ndani ya ukumbi.
Alisema
licha ya kwamba Mwenyekiti wa CCM Rais Magufuli. amekataza mikutano
hiyo kufanyika chama tawala, kinafanya mikutano ya hadhara katika maeneo
mbalimbali kwa kisingizio cha shughuli za serikali.
Mabina
alisema juzi CCM ilisema itakuwa na maandamano kutoka uwanja wa ndege
wa Mwalimu Nyerere ya kumpokea Rais Magufuli hadi Makao Makuu ya CCM
yaliyopo Lumumba.
“Tunahoji
haki ya kufanya siasa ni kwa CCM tu na siyo kwa vyama vingine? Hili
jambo hatuwezi kukubali Jeshi la Polisi lituambie inakuwaje vibali
vinatolewa kwa CCM halafu upinzani tunyimwe tunasema lazima tufanye
oparesheni Ukuta ya kupinga ukandamizaji wa demokrasia,” alisema Mabina
Naye
Katibu wa Wabunge wa Upinzani Mkoa wa Dar es Salaam, Mbunge wa Viti
Maalum, Anatropia Theonest, alisema lengo la oparesheni ya Ukuta ni
kupinga ukandamizaji unaofanywa na serikali.
Alisema
wana haki ya kikatiba ya kufanya mikutano bila kuzuiliwa kama ambayo
wamefanyiwa na ndio maana wameanza kugawa bendera kwa ajili ya kujiandaa
na oparesheni hiyo.