test

Ijumaa, 12 Agosti 2016

Chadema Inavyopangua Kete za CCM> soma hapa



Wakati Serikali ya CCM imekuwa ikijenga mazingira ya kuzuia uwezekano wa vyama vya upinzani kufurukuta, Chadema imekuwa ikichanga karata zake na kuendelea kujiimarisha na kushindana kisiasa na chama tawala.

Kwa mujibu wa baadhi ya wasomi na wanasiasa nchini, matukio makubwa ya kisiasa yanayoandaliwa na Chadema na kuibua mijadala imekuwa ikifanywa kimkakati sambamba na ya chama tawala, CCM.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Richard Mbunda aliliambia Mwananchi kwamba aonavyo yeye matukio mbalimbali ya Chadema ni mikakati ya kisiasa. “Inabidi wafanye matukio ili chama kiendelee kubaki katika ramani ya siasa,”alisema Mbunda.

Mwenyeki wa Chadema, Freeman Mbowe amesema tofauti na mawazo ya baadhi ya watu, matukio hayo zikiwamo operesheni mbalimbali za chama si mikakati ya kudumu bali ni za muda maalumu kwa malengo maalumu ambayo ikikamilika wanabuni mbinu nyingine.

Chadema wamekuwa wakibuni mikakati mbalimbali ya kuwafikia wananchi tangu mikutano na maandamano ya vyama vya siasa ilipopigwa marufuku na Rais John Magufuli hadi mwaka 2020. Mikutano iliyoruhusiwa ni ya wabunge tu tena katika majimbo yao, lakini si ya wanasiasa.

Katika Bunge la Bajeti, wabunge wa Chadema wakishirikiana na wenzao kutoka vyama vya siasa vinavyounda Ukawa walikuwa wakisusa vikao kwa staili tofauti. Kuna siku walitoka nje wakiwa wamevaa mavazi meusi, siku nyingine walibandika vitambaa mdomoni na kuna siku walibeba mabango yenye ujumbe mbalimbali.

Julai mwaka huu, CCM ilipoandaa mkutano maalumu uliopangwa kwa ajili ya kumkabidhi Rais Magufuli kijiti cha uenyekiti wa chama hicho, Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha) lilizua hofu lilipotangaza kwamba litakwenda pia Dodoma kulisaidia Jeshi la Polisi kuzuia mkutano huo kwa kuwa Serikali ilipiga marufuku mikutano ya ndani na nje.

Hatua hiyo ya Bavicha ilisababisha Jeshi la Polisi kuweka ulinzi mkali kila kona mjini Dodoma kuzuia uwezekano wa Bavicha kuvuruga mkutano huo wa CCM. Hata hivyo, Bavicha walipiga chenga, walikutana Dar es Salaam ambako walifanya mkutano wao.

Wajumbe wa mkutano mkuu wa CCM walipokuwa katika shangwe na nderemo baada ya kukamilisha ajenda yao ya kumchagua kwa asilimia 100 Rais Magufuli, Kamati Kuu ya Chadema iliketi Dar es Salaam na kutoka na mkakati wa kupinga uvunjaji wa Katiba na sheria waliouita operesheni Ukuta ambao unasumbua vyombo vya usalama hadi sasa.

Matukio hayo ambayo yametokea kwa kufuatana yamekuwa yakigonga vichwa vya habari huku baadhi wakidai ni dalili za vurugu na uchochezi, lakini pia yanakiweka chama hicho kwenye mjadala kuliko vingine.



Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa waliotafutwa na gazeti hili jana kuzungumzia namna Chadema inavyocheza karata zake kuhakikisha inasikika sawa au hata kuifunika CCM, wamesema huo ni mkakati wa upinzani kuendelea kutamba kwenye ‘ulingo wa siasa.’ Baadhi ya operesheni zilizoijengea umaarufu ni kama Sangara na Movement For Change (M4C).

Akizungumzia mfuatano wa matukio hayo, Mbunda amesema aonavyo yeye matukio hayo ni mikakati ya kisiasa akibainisha kuwa kila chama kina wapangaji mikakati ambao hupanga na kutathmini mikakati hiyo. “…Siyo mikakati yote inayofaulu. Wakiona huu haufai wanaweza kubadili.”

Mhadhiri huyo alitoa mfano wa Operesheni Ukuta ya Chadema iliyopangwa kufanyika Septemba Mosi mwaka huu kwamba huenda wakati ukifika chama hicho kikabadili uamuzi wake baada ya kufanya tathmini ya operesheni hiyo.

Mbunda amesema kwamba hizo ni amsha amsha ambazo husaidia vyama hasa vya upinzani kuendelea kuonekana katika uso wa siasa na kwamba vyama mbalimbali duniani hutumia mbinu hizo hivyo siyo jambo la kushangaza. “Wasipofanya hivyo hata watu watahoji kwa sababu hayo ndiyo maisha ya siasa,”alisema Mbunda.

Kauli hiyo iliungwa mkono na Dk Benson Bana ambaye alisema kinachofanywa sasa na Chadema ni mkakati wa kuendelea kubaki na kusikika kwenye uwanja wa siasa.

Dk Bana, ambaye ni mhadhiri wa UDSM amesema chama hicho kinafanya hivyo ili kisipotee kwenye ramani ya siasa hadi Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

Mchambuzi huyo wa masuala ya siasa alibainisha kuwa chama hicho kikuu cha upinzani kinafanya hivyo kwa sababu kilikuwa hakijajipanga kuona Serikali ya awamu ya tano inatekeleza baadhi ya ajenda zao.

“Hawajajipanga kuwa na mikakati endelevu…wanaona wamenyang’anywa tonge mdomoni. Mikakati yao ni ya kuziba ombwe hilo,” alisema.

Pia, Dk Bana amesema  jambo hilo siyo baya kwenye ulimwengu wa siasa tatizo ni aina ya mikakati kwamba Chadema inapaswa kuja na mikakati ambayo inakidhi haja ya Watanzania siyo mikakati ya kumwita Rais John Magufuli dikteta. “Watathmini mikakati yao. Waje na mikakati yenye mashiko,”amesema Dk Bana.

Install Application ya JUNGUKUULEO Uweze Pata Habari Kirahisi Zaidi

xxxxxxxxxxxxx