Habari/Picha Na Jonas Kamaleki
Ofisi
ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu,Bunge, Kazi, Ajira na Watu Wenye Ulemavu
itahamia Dodoma juma lijalo kufuatia agizo la Mhe. Rais John Pombe
Magufuli la Serikali kuhamia Dodoma........
Kauli
hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Waziri wa Nchi Ofisi ya
Waziri Mkuu, Sera, Uratibu, Bunge, Kazi ,Ajira, Vijana na Watu wenye
Ulemavu, Jenista Mhagama wakati akiongea na watumishi wa Ofisi ya Waziri
Mkuu na Taasisi zilizoko chini ya ofisi hiyo.
“Mchakato
wa kuhamia Dodoma umekwisha kilichobaki kwa sasa ni utekelezaji, mimi
na manaibu mawaziri wangu tunahamia juma lijalo ili tukamkaribishe Mhe.
Waziri Mkuu anayehamia Septemba mwaka huu,” alisema Mhagama.
Mhagama
amesema kuwa kila kiongozi anayehamia Dodoma inabidi awakute walio
chini yake tayari wamekwishahamia ili kumpokea, hivyo akawataka na
watendaji ambao wako chini yake watangulie kwa ajili ya kumpokea yeye na
viongozi wenzake.
Aidha, Waziri huyo amesema kwa sasa hakuna mjadala wa kuhamia Dodoma lilobaki ni utekelezaji tu wa kuhamia Makao Makuu.
Mhagama
amesema kama kuna Taasisi chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu imetenga fedha
kwenye bajeti kwa ajili ya ujenzi, shughuli hiyo ikafanyike Dodoma
ambako Serikali inahamia. Kwa kusema hivyo kadhalika na ofisi au Wizara
nyingine za serikali ambazo zimetenga fedha ya ujenzi wakajenge Dodoma.
Suala
la kuhamia Dodoma sio geni bali limekewepo kwa kipindi kirefu ila
utekelzaji wake ndio ulikuwa bado; pia katika Ilani ya uchaguzi ya CCM
ya mwaka 2015 suala hili lipo, alisema Mhagama na kuongeza kuwa kipindi
cha nyuma Wizara saba (7) ziliwahi kuhamia Dodoma na kwa sasa Wizara
inayoshughulikia Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) iko
Dodoma.
Waziri
Mhagama ameipongeza Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kuanza ujenzi wa
jengo lake mjini Dodoma na kusisitiza kuwa Wizara na Taasisi nyingine za
Serikali kuiga mfano huo kwa kujenga ofisi zao Dodoma.
“Kwa
kuwa sisi ni waratibu wa wizara zote inabidi tuunde kikosi kazi
kitakachofanya kazi ya uratibu wa kuhama kikiwa Dodoma ili kuwawezesha
na watumishi wenzetu kutekeleza agizo la Mhe. Rais la serikali nzima
kuhamia huko,”alisema Mhagama.
Mhagama
amesema kuwa Mamlaka ya Ustawishaji wa Makao Makuu Dodoma (CDA)
wameshafanya kazi nzuri ya upimaji eneo la serikali ambalo litatumika
kwa ajili ya ofisi.
“Tumefika mwisho wa mchakato sasa ni utekelezaji na tunataka watumishi walielewe vizuri suala hili na wawe tayari kulipokea,”alisisitiza Mhagama.
Kuhamia
Dodoma katika kipindi hiki kunatokana na agizo la Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli alillolitoa tarehe
25 Julai, 2016 mjini Dodoma kwenye Mkutano Mkuu Maalum wa CCM ambao
ulimchagua kuwa Mwenyekiti wa tano wa chama hicho tawala.