MAMIA
ya wananchi wameanza kupeleka maombi ya viwanja katika ofisi za Mamlaka
ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA), imeelezwa.
Hali
hiyo imetokea baada ya Rais Dk. John Magufuli kutangaza nia ya Serikali
kuhamia mjini hapa kwa kuwa ndiko yaliko makao makuu ya nchi.
Kutokana
na idadi kubwa ya watu wanaofika katika ofisi za Idara ya Ardhi katika
mamlaka hiyo, Jeshi la Polisi mkoani hapa limelazimika kuimarisha ulinzi
ili kukabiliana na hali hiyo.
Mmoja
wa watu waliokutwa ofisini hapo na kujitambulisha kwa jina la Salum
Kijuu, mkazi wa Area A, alimwambia mwandishi wa habari hizi
aliyeshuhudia mamia ya watu ofisini hapo jana, kwamba alifika ofisini
hapo kulipia kiwanja chake kilichopo eneo la Miganga.
“Kaka
hii foleni ya watu karibia wote wanaulizia viwanja, mimi nimekuja
kulipia kiwanja changu ili niweze kukimiliki kihalali kwani mambo
yameshabadilika,” alisema Kijuu.
Wakati
hali ikiwa hivyo, Mkurugenzi Mkuu wa CDA, Paskasi Muragili, alisema
ardhi mjini hapa itauzwa kwa bei ya kawaida ili watu wengi waweze
kumiliki viwanja.
“Kwa
mfano, ‘square’ mita moja ya kiwanja cha makazi itauzwa kwa Sh 5,500
hadi Sh 10,000 katika maeneo ambayo kitaalamu tunayaita ‘medium
density’.
“Kwa sasa maeneo yanayouzwa ni Miganga na Mkalama yaliyopo nje kidogo ya mji wa Dodoma.
“Viwanja
kwa ajili ya uwekezaji mkubwa ‘square’ mita moja itauzwa kwa Sh 13,300
na maeneo hayo kitaalamu tunayaita ‘low density’.
“Pamoja
na uwepo wa mahitaji makubwa, nasema ardhi ipo ya kutosha, yaani hata
kama watakuja wananchi wote wa Dar es Salaam, watapata ardhi ya kutosha.
“Narudia
tena, ardhi ipo ya kutosha, hata kama watu watakuja baada ya miaka 30,
wataipata kwa sababu hata Mwalimu Nyerere alipoamua Dodoma iwe makao
makuu, alijua kuna ardhi ya kutosha kwa idadi yoyote ya watu,” alisema Muragili.
Akizungumzia
mpangilio wa mji utakavyokuwa, alisema mji wa kiserikali utaanzia
katika Kijiji cha Mtumba hadi eneo la Ikulu ndogo ya Chamwino, ambako
kutakuwa na ofisi za wizara na mabalozi.
“Mji
wa kibiashara, utakuwa ni eneo lote la mji wa Dodoma kwa sababu hii
ramani ninayokwambia iko katika ‘master plan’ ya mwaka 2010-2030 ya
kuhakikisha makao makuu ya nchi yanakuwa vizuri kuanzia kwenye barabara
za kuingia na kutoka ili kusiwe na msongamano wa aina yoyote,” alisema.
Pamoja
na hayo, mkurugenzi huyo alitoa angalizo kwa wanaohitaji kununua
viwanja mjini Dodoma na kusema watatakiwa kupitia CDA kwa kuwa ndiko
vinakopatikana.
“Viwanja
tusinunue kienyeji, tufuate taratibu kwani najua watatokea wapigaji wa
dili watakaowaumiza watu. Nawaombeni mje ofisini kwetu, kama mnataka
viwanja mtapata tu kwa kufuata utaratibu,’’ alisema.
Naye
Ofisa Uwekezaji wa CDA, Abeid Msangi, alisema wametenga maeneo maalumu
ya Itega na Njendengwa kwa ajili ya kujenga mahoteli makubwa na nyumba
mbalimbali za kupanga.
“Lakini kwa sasa eneo la Itega limeshajaa, ila Ndejengwa tumetenga zaidi ya ekari 1,500 kwa ajili ya uwekezaji mkubwa.
“Kuonyesha
kwamba tulijipanga mapema katika eneo la uwekezaji, kule Ndejengwa
miundombinu iliishafika mapema, kwani kuna maji, umeme pamoja na
barabara za lami,” alisema Msangi.
Hivi
karibuni, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo,
alisema watazalisha umeme wa megawati 60 ili kuondoa tatizo la kukatika
kwa umeme katika Mkoa wa Dodoma.
Profesa
Muhongo alitoa kauli hiyo hivi karibuni alipofanya ziara ya kukagua
maendeleo ya mradi wa kujenga njia ya kusafirisha umeme wa kilovoti 400
kutoka Iringa hadi Shinyanga kupitia Dodoma na Singida.
Naye
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka, Mkoa wa Dodoma
(Duwasa), David Pallangyo, ameshasema wamejipanga kuhakikisha maeneo
yatakayopimwa, yanapata maji safi na salama.
Kwa
upande wake, Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Mkoa wa
Dodoma, Bernard Chimagu, naye alishasema wamejipanga kukabiliana na
ongezeko la magari.