![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEj3sFYBhfdvfrQx2OCnCeSKcy1VHEBtNpVOGU1JMpJ7a4YtlfxZYuuDCafKaiUP5kfqD3t7jDBPdSzrlTyhjAExl3K_-4bdaTo0neaPN32zFbPXftawFXRhVPEU-4lfmdQS7VzQffw9OrO9/s640/1.jpg)
Mwenyekiti
mwenza wa Ukawa James Mbatia amesema wameamua hawatasalimiana na
wabunge wa CCM, wala kushirikiana nao kwenye shughuli mbalimbali.
Hata
hivyo, Nsanzugwako alisema jana kuwa hawezi kufahamu kama mawazo yake
aliyowahi kuyatoa bungeni wakati akichangia hotuba ya bajeti kuu mwaka
2016/17 yamefanyiwa kazi.
“Bado
ninaamini katika kukaa pamoja na kujadiliana, miye ni muumini wa
reconciliation (upatanishi) na Bunge ni taasisi siyo mtu binafsi
hatuwezi kukaa sisi wanaCCM pekee yetu,” alisema Nsanzugwako.
Akichangia
katika hotuba ya bajeti wiki iliyopita, Nsanzugwako alimshauri Dk
Ackson kuwasamehe wabunge wa kambi ya upinzani na wakae meza moja
kujadiliana na kuondoa tofauti zao.
Nsanzugwako
alihoji faida wanayoipata wabunge wa CCM kwa wabunge wa Kambi ya
Upinzani kususa vikao vinavyoendeshwa na Naibu Spika, Dk Tulia Ackson.
Kauli
hiyo ilionekana kutowafurahisha wabunge wa CCM na Mbunge wa Mtera
(CCM), Livingstone Lusinde alimpatia taarifa Nsanzugwako kuwa hakuna
mbunge wa upinzani aliyefukuzwa na Naibu Spika na kwamba kumuomba Dk
Tulia awasamehe ni kuondoa ukweli kwamba wabunge wameadhibiwa na Bunge
zima na siyo Naibu Spika.
Dk Tulia alisema hakuna mbunge aliyefukuzwa ila wabunge hao wameamua kuondoka kwa utashi wao wenyewe.
Alisema kanuni ya tano ya Bunge imetoa mwongozo wa jinsi ya kuwasilisha malalamiko ya wabunge wanapokuwa na jambo na kiti.
Alisema
tayari wabunge wa kambi hiyo wamewasilisha malalamiko yao jambo ambalo
ni haki yao kimsingi . Alisema katika Bunge lililopita wapinzani
waliwahi kutumia kanuni hiyo kuwasilisha malalamiko yao dhidi ya kiti,
lakini hawakususia vikao vya Bunge.
"Napenda
kumfahamisha mheshimiwa mbunge kuwa hakuna mtu waliyemuudhi wala
wanaohitaji kuomba msamaha. Wao wametoka kwa utashi wao,”alisema.
Katibu
wa wabunge wa CCM, Jasson Rweikiza, alisema hizo ni fujo tu za wabunge
wa Kambi Rasmi ya Upinzani na kwamba hakuna kitu wanachopoteza kwa wao
kutoka nje ya Bunge.
Alisema
kanuni zinajieleza jinsi ya kufanya iwapo kuna mbunge hakubaliani na
kiti cha Spika kwa kupeleka malalamiko yake katika Kamati ya Haki,
Maadili na Madaraka ya Bunge.
“Sisi
tutafanyaje sasa kama watu wameamua kufanya fujo, sisi tumeendelea na
shughuli za Bunge kwa kujadili kwa kina hotuba zote na kutoa mapendekezo
yetu,” alisema.
Alisema
kutoka kwa wapinzani hakuna jambo lilipungua kwani mambo yote
yamekwenda sawa na sasa watajadili Muswada wa Sheria ya Fedha ya mwaka
2016 ambayo tayari wabunge wa CCM wamepeleka majedwali ya marekebisho.
“Sisi hatuwezi kumlazimisha mtu atupende. Kutoshiriki kwao vikao kunaondoa maana nzima ya kuwa wabunge. Safari ijayo wananchi wasiwachague hawa wahuni, wawachague wabunge wanaotokana na CCM,” alisema.
Hata
hivyo, katika kikao cha wabunge wa CCM walichofanya katika ukumbi wa
Pius Msekwa na kuongozwa na Mwenyekiti wao Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
jana wabunge walijadili mambo mawili.
Miongoni
mwa mambo hayo ni hofu waliyonao baada ya wabunge wa upinzani kukataa
kusalimiana nao na kushirikiana nao kwenye shughuli mbalimbali na
kuelezwa kwanini muswaada wa Sheria ya Fedha haujaenda bungeni hadi
sasa.
Wabunge
hao walielezea hofu waliyonayo juu ya kufanyiwa vitendo vibaya na
wabunge wa kambi ya upinzani. Majaliwa aliwaondoa hofu wabunge hao na
kwamba hawana haja ya kuwa na hofu kwa sababu nchi iko salama.
Hata hivyo, aliwataka kuwa wavumilivu na kuendelea kushirikiana nao.