MSAFARA wa mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, umenusurika kupata ajali, baada ya lori la mizigo kuuvamia na kugonga magari matatu likiwamo lililokuwa limembeba mpiga debe wa chama hicho, Amon Mpanju.
Ajali hiyo ilitokea jana asubuhi katika eneo la Njia Panda jirani kilomita chache kabla ya kuingia Maswa mjini.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Gemin Mushi jana alikiri kutokea kwa tukio hilo.
Alisema
wakati msafara huo ukitoka wilayani Meatu, askari polisi waliokuwa
wakiuongoza msafara huo walimuaru dereva wa lori hilo lenye namba za
usajili T 217 DDY kuegesha pembeni gari lake, lakini alikaidi.
“Msafara
wa mgombea urais ulikuwa jirani kuingia Maswa, dereva wa lori
aliamuriwa kuliweka pembeni akakaidi, tena kibaya akaongeza mwendo hali
iliyosababisha ajali.
“Lori
hili ni mali ya Kampuni ya Dilchadri Mill Ltd ya jijini Mwanza,
liligonga magari matatu likiwamo gari lenye namba za usajili T 217 CYM
aina ya Toyota Land Cruser ambayo iliharibika vibaya na kushindwa
kuendelea na safari.
“…Baada ya tukio hili, dereva amekimbia na polisi wanamsaka ili afikishwe mbele ya vyombo vya sheria,” alisema Kamanda Mushi.
Kutokana
na ajali hiyo, Kamanda Mushi amewataka madereva kuzingatia sheria za
usalama barabarani.Alisema hakuna mtu aliyeumia katika ajali hiyo.
Wakati huo huo, mgombea huyo aliendelea na mikutano yake katika wilaya za Maswa, Kishapu na Igunga.
Kwa
nyakati tofauti katika mikutano hiyo, Dk. John Magufuli, aliwataka
Watanzania kuchagua wabunge ambao watatetea masilahi yao badala ya wale
wanaotoka bungeni kila zinapowasilishwa bajeti.
Alisema endapo atachaguliwa anataka kuona Bunge linalotimiza wajibu wake, ikiwemo kupigania kero za waliowachagua.
“Haiwezekani wakati wa kujadili hoja za wananchi, wenzako wanatoka nje wanafanya hivi kwa kumkomoa nani?
“Maswa
ninyi ni mashahidi kwa muda mrefu hamkuwa na mtu wa kuwasemea tatizo la
maji, barabara na hata huduma za afya. Maana kila zinapopangwa bajeti
wao wanatoka nje je waziri atajuaje kama kuna tatizo eneo husika.
“Hii
si demokrasia hata kidogo ila ni kuwatesa wananchi, kwa hali hiyo sasa
Watanzania wote chagueni wabunge wenye masilahi kwenu na watakaosemea
shida zenu na si wale wanaotoka nje kila wakati (Ukawa),” alisema Dk. Magufuli
Aonya lugha chafu
Alisema ni vema viongozi wa vyama vya siasa kuepuka kampeni za matusi, kwani hazina tija kwa Taifa.
“Matusi
si hoja, ndiyo maana kila ninaposimama situkani mtu, najenga hoja.
Tunahitaji kujenga nchi yetu iwe ya amani siku zote,” alisema.
0 comments:
Chapisha Maoni