test

Jumapili, 16 Agosti 2015

Hali ni tete CCM!! NAPE: "WALIOHAMA,WANAOHAMA NA WATAKAOHAMA HILI SIYO JAMBO JIPYA",AFICHUA SIRI YA MGEJA KUMFUATA SWAHIBA YAKE LOWASSA




Hali inazidi kuwa tete ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) baada ya vigogo tisa, akiwamo Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana mkoani Kilimanjaro (UVCCM), Fredy Mushi , jana kujiuzulu nyadhifa zao na kutangaza kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).


Wengine waliotimka ni Katibu wa Uchumi na Fedha na Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa (CCM), Paul Matemu, Mchumi wa UVCCM mkoa wa Kilimanjaro, Jerome Komu na Noel Nnko ambaye alikuwa Mratibu wa Kanda ya Kaskazini wa Marafiki wa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, wamo pia Wafanyabiashara maarufu wa mikoa ya Arusha na Kilimanjaro, Douglas Malamsha na Peter Kirenga. Wengine ni pamoja na Goreth Augustino na Hadija Msuya.

Akitangaza hatua hiyo jana, Fredy alisema kwa sasa ndani ya CCM ili upate nafasi ni lazima kujipendekeza kwa watoto wa vigogo au kuwakebehi wazee wanaochukizwa na hatua ya kuvunjwa kwa demokrasia.
Kujitoa kwa vigogo hao, kumefanya idadi ya makada waandamizi waliokihama CCM ndani ya mwezi mmoja kufikia 21.

NAPE: CCM HAKISHTUSHWI
Katibu wa Nec, Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, amesema CCM hakishtushwi na makada na viongozi wanaoendelea kukihama chama hicho na kujiunga na Chadema na kudai kuwa wanao ondoka wana sababu zao binafsi.

Amesema hakuna kiongozi wa upinzani ambaye hakuanzia CCM hivyo ni hali ya kawaida kwa chama kikubwa kama hicho ambacho kina mtaji wa wanachama takribani milioni nane, makada wake kuhama.


Nnauye alisema hayo jana wakati akitoa ufafanuazi wa masuala mbalimbali yanayokihusu chama hicho kwa waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam.

“Waliohama, wanaohama na watakaohama hili siyo jambo jipya lilishatokea tangu miaka 23 iliyopita na litaendelea kwa muda mrefu hivyo siyo jambo la kushangaza, kuna viongozi wakubwa waliondoka na wengine wakarudi, Mfano Maalim Seif na Agustine Mrema walikuwa CCM na waliondoka.”

Kuhusu kuondoka kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja na kujiunga na Chadema alisema, “Mgeja alitegemewa kuondoka muda mrefu kutokana na uswaiba wake na Edward Lowassa lakini alichelewa kwa sababu alikuwa anasubiri mtoto wake aliyegombea viti maalum aliyekosa kura, hivyo alitumia nafasi yake kushawishi viongozi wa chama wampitishe na alipoona ameshindwa aliamua kutimiza azma yake ya siku nyingi ya kukihama chama,”

Akimzungumzia aliyekuwa Mwenyekiti wa Vijana UVCCM na Mwenyekiti mstaafu wa CCM mkoa wa Dar es Salaam, John Guninita, alisema aligombea ubunge Jimbo la Kilombero lakini alishindwa hivyo kwa hasira akaamua kuondoka na kujiunga na Chadema.

Aidha, alikanusha taarifa zinazosambaa mitandaoni kuwa, Mgombea urais wa CCM, Dk.John Magufuli, alitangaza kuwagawia kompyuta walimu wote.

Alisema taarifa hizo ni za uzushi na kwamba Ilani ya uchaguzi ya chama hicho ilipitishwa juzi mkoani Dodoma na inatarajiwa kuzinduliwa Agosti 23, mwaka huu.

Kamati Kuu ya CCM (CC) ilitengua matokeo ya majimbo matano yaliyowapa ushindi mawaziri watatu waliokuwa wakitetea ubunge katika majimbo yao katika kura za maoni kwa madai ya kujitokeza dosari mbali mbali za uchaguzi.

Majimbo yaliyorudiwa kuanzia Agosti 12 na Agosti 13 ni Kilolo (Iringa), Busega (Simiyu), Ukonga (Dar es Salaam), Rufiji (Pwani) na Makete (Njombe).

Jumanne wiki hii Nape alitangaza kurudiwa kwa uchaguzi huo baada ya Kamati ya Usalama na Maadili ya chama hicho iliyokutana Agosti 7, kuchambua rufaa hizo, kufuatia malalamiko kadhaa yaliyowasilishwa na wagombea.

Ingawa dosari zilizojitokeza katika uchaguzi huo hazikutajwa lakini malalamiko makubwa yaliyojitokeza ni uchakachuaji wa kura na kukithiri kwa vitendo vya rushwa.

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanaeleza kuwa kama dosari hizo zimeanza kujitokeza katika kura za maoni tena ndani ya chama tawala, kuna wasiwasi dosari nyingi zinaweza kuibuka katika Uchaguzi Mkuu.

MAONI YA WADAU
Shekhe wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhaji Musa Salum, anasema kiongozi atakayechaguliwa kwa misingi ya rushwa ni dhahiri hataheshimu raia na ataliongoza taifa kwa dhana ya kuwanunua watu na kujilimbikizia mali.
“Kiongozi wa namna hii lazima ahakikishe fedha alizotumia kuwahadaa wananchi anazirudisha kwa namna yoyote ile,” anasema.

Shekhe Salum anasema kwa kiwango fulani Takukuru imetimiza wajibu wake na ameshuhudia wakubwa wamekamatwa ingawa hawajathibitishwa kutenda kosa.

“Dhambi ya rushwa ina pande mbili ndio maana sheria ya dini inasema mtoa rushwa na mpokea rushwa wote wanaenda motoni bahati mbaya sheria zetu za nchi zinawatizama watoaji huku mpokeaji akionekana hana hatia.”

Aidha, anasema lazima ifike mahali wananchi waelewe kuwa rushwa ni haramu na yeyote atakayepokea ashughulikiwe ipasavyo.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Benson Bana, kwa upande wake anaeleza kuwa, kutokana na matumizi ya fedha kuwa makubwa kwenye vinyang’anyiro hivyo, yamehalalisha vitendo hivyo viovu kuonekana mbele ya jamii kama ni halali.

Anaeleza kuwa nguvu ya fedha imekuwapo kwa sababu wale wanaowania nafasi ya ubunge wanatambua mara baada ya miaka kumi wanaondoka na kiinua mgongo kikubwa.

“Rai yangu ni wabunge walipwe viinua mgongo vyao mara baada ya uchaguzi kuisha badala ya mfumo wa ulipaji baada ya kuvunjwa kwa bunge, hii itawaondolea kiburi cha fedha,” alisema.

Hata hivyo, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), ilipotakiwa kuzungumzia tatizo hilo ilishauri isubiriwe uchaguzi utakapomalizika ndipo itoe tathmini yake.

Wakili wa kujitegemea, Emmanuel Safari, akizungumzia sheria ya gharama ya uchaguzi anasema, kazi yake ni kudhibiti matumizi ya fedha katika uchaguzi.

Alisema sheria hiyo inatamka wazi kuwa, mgombea anatakiwa kuwa na bajeti yake na aonyeshe anazipataje fedha hizo.

"Sheria hiyo inatoa haki kwa mgombea kusafiri na wapambe wake kwa mfano madereva, wanaokubebea vitu, kama una kikundi cha kuhamasisha, hawa sheria hii inaruhusu kuwalipa, lakini wale mashabiki wa kisiasa wanaosafirishwa kutoka eneo moja hadi lingine na kulipwa, sheria haiwatambui, lakini mambo mengine ili uthibitishe kuwa ni rushwa wanaohusika ni Takukuru," alisema.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Ally, Bashiru kwa maoni yake anasema rushwa bado inatukuzwa kwa kuwa bila pesa huwezi kupata uongozi.

Alisema wala rushwa wanatukuzwa kwa sababu jamii haijaamuua kuwachukulia hatua ikiwemo kuwazomea ama kuwatenga kama watu ambao wanautaka uongozi kwa rushwa.

Alisema Takukuru inawatuhumu tu watu hao, bado hawajathibitishwa na mahakama, wangechukuliwa hatua ingesaidia baadhi ya watu wanaotaka uongozi wa kutoa fedha kuogopa kufanya hivyo.

“Hatujawahi kukaa chini kumaliza ugonjwa huo watu wanakubali kununuliwa bila kujua athari zake ni zipi,” alisema

Alisema waliotuhumiwa kwenye sakata la Escrow wamepitishwa kugombea na vyama vyao na wananchi wameshindwa kuwahoji.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Profesa Abdallah Safari, amesema wagombea wanaotoa rushwa katika kipindi hiki cha uchaguzi hawajiamini, hivyo wanatoa fedha ili wachaguliwe.

Prof. Safari ambaye pia ni mwanasheria kitaaluma, alisema sheria ya uchaguzi ipo wazi kwa yeyote ambaye atabainika kutumia rushwa na mahakama ikathibitisha uongozi wake hutenguliwa kama ilivyo kwenye katika kesi ya Igunga.

MAKADA WALIOTIMKA
Vigogo wengine waliotangulia awali kujitoa na kujiunga na Chadema ni Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowasa, Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Arusha, Onesmo Ole Nangole, Katibu wa Itikadi na Uenezi mkoa huo, Isaac Joseph, maarufu kama Kadogoo na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Sumbawanga Mjini, Emanuel Kilindu.

Yumo pia Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja na Mwenyekiti Mstaafu wa CCM, mkoa wa Dar es Salaam, John Guninita.

Wabunge waliomaliza muda wao na kujiunga Chadema ni Mbunge wa Kahama Mjini, James Lembeli, Arumeru Mgaharibi Goodluck Ole Medeye, Segerea, Dk. Makongoro Mahanga; Sikonge, Said Nkumba na Viti Maalum, Esther Bulaya.

*Taarifa hii imeandikwa na Godfrey Mushi (Moshi), Romana Mally, Beatrice Shayo, Mary Godfrey (Dar es Salaam-NIPASHE

Install Application ya JUNGUKUULEO Uweze Pata Habari Kirahisi Zaidi

xxxxxxxxxxxxx

0 comments:

Chapisha Maoni