BEKI Mtanzania anayekipiga katika Klabu ya Baroka ya Afrika Kusini,
Abdi Banda, ameweka bayana kwamba hadi sasa ana ofa za timu 15 ambazo
zinahitaji saini yake baada ya kufanya vizuri katika msimu wake wa
kwanza nchini Afrika Kusini.
Banda amekuwa na msimu mzuri katika kikosi cha Baroka FC kwa
msimu uliomalizika hivi karibuni wa Ligi Kuu ya Afrika Kusini (PSL),
ambapo amechangia kwa kiasi kikubwa kuibakisha timu hiyo isishuke
daraja.
Beki huyo ndani ya msimu wake wa kwanza akiwa huko amefanikiwa
kucheza jumla ya mechi 39 za michuano yote kwa timu hiyo na alichaguliwa
mara mbili kuwa mchezaji bora wa timu yake wa mwezi.
Banda amesema timu
hizo ni za kutoka ndani na nje ya Afrika Kusini ambazo zinamhitaji baada
ya kuonyesha uwezo ndani ya kikosi chake cha Baroka alichojiunga nacho
akitokea Simba.
“Hadi sasa kuna timu 15, ambazo zimeonyesha nia ya kunihitaji kwa
ajili ya kuzichezea kwa msimu ujao, ambapo mambo yote yanasimamiwa na
wakala wangu ambaye ndiye msimamizi wa kila kitu kwangu.
“Zote hizo zimekuja kwa sasa baada ya kuonyesha uwezo nikiwa Baroka
FC, ikizingatiwa huu ndiyo kwanza msimu wangu wa kwanza kucheza katika
ligi na timu hiyo,” alisema Banda.
Wakala wa Banda, Paul Mitchell, kutoka Kampuni ya Siyavuma Sports
Group, alisema: “Banda ni mchezaji mzuri na amekuwa na kiwango kikubwa
katika msimu wake wa kwanza akiwa hapa. Ni kweli kuna timu ambazo
zimeonyesha nia ya kumtaka kwa ajili ya msimu ujao lakini kwa sasa
siwezi kusema ni timu gani hizo.”
0 comments:
Chapisha Maoni