Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli
amewataka Wabunge wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kutilia mkazo ajenda
zitakazoimarisha zaidi umoja, upendo, ushirikiano na mshikamano baina ya
nchi wanachama ili kufanikisha jukumu muhimu la kupambana na umasikini
wa wananchi na kukuza uchumi.
Mhe.
Rais Magufuli amesema hayo tarehe 24 Aprili, 2018 wakati akihutubia
Bunge la Afrika Mashariki kwa mara ya kwanza tangu aingie madarakani,
katika ukumbi wa Pius Msekwa uliopo ndani ya viwanja vya Bunge Mjini
Dodoma ambako Bunge hilo linafanyia vikao vyake kwa mara ya kwanza
katika mji huo.
Mhe.
Rais Magufuli amesema Wabunge hao wanao wajibu wa kushughulikia
migogoro ambayo imekuwa ikigharimu maisha ya wananchi, vikwazo vya
biashara na uwekezaji, na kutilia mkazo ujenzi wa viwanda
vitakavyochakata na kuzalisha bidhaa zitokanazo na rasilimali lukuki
zilizopo ndani ya Afrika Mashariki ili manufaa ya rasilimali hizo
yawanufaishe wananchi.
Ametaja
miongoni mwa mambo yanayopaswa kutiliwa mkazo na nchi zote kuwa ni
kuimarisha miundombinu ya usafirishaji na uzalishaji wa umeme wakutosha
na wenye gharama nafuu, ambavyo ni muhimu katika ujenzi wa viwanda.
“Tafiti
zinaonesha gharama za usafiri kwenye ukanda wetu ni mara 4 hadi 5
ukilinganisha na gharama za Asia Mashariki, Marekani na Ulaya na
zinachangia kuongezeka kwa gharama za bidhaa kwa asilimia 40.
“Umeme
pia umeonekana kuwa sio mwingi, utafiti uliofanywa na taasisi ya Power
Africa mwaka 2015 umeonesha kuwa nchi zote 6 za Jumuiya ya Afrika
Mashariki zina takribani megawati 6,500 tu za umeme, hiki ni kiwango
kidogo mno kuweza kuhimili mahitaji ya uchumi wa kisasa” amesisitiza
Mhe. Rais Magufuli.
Katika
kutekeleza azma hiyo Mhe. Rais Magufuli ametoa wito kwa nchi wanachama
kubadilishana uzoefu wa namna ya kukabiliana na changamoto mbalimbali
zinazojitokeza na kutekeleza miradi muhimu ya maendeleo, na pia
ameshauri nchi wanachama zisitegemee misaada pekee na badala yake
zifikirie kutekeleza miradi kwa fedha zake zenyewe ili kuokoa muda na
kupunguza gharama za miradi husika.
Mhe.
Rais Magufuli amezungumzia juhudi zinazofanywa na Tanzania katika
kufikia dhamira hiyo kuwa ni pamoja na kuanza ujenzi wa reli ya kisasa
(Standard Gauge) kuanzia Dar es Salaam hadi Dodoma ambayo itaunganisha
hadi nchi za Burundi, Rwanda na Uganda, kujenga meli katika ziwa
Victoria, kutekeleza mradi wa uzalishaji wa umeme katika mto Rufiji
(Stieglers’ Gorge), kununua ndege 6, kujenga barabara, kupanua bandari
ya Dar es Salaam, ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka
Hoima nchini Uganda hadi bandari ya Tanga nchini Tanzania, kuboresha
viwanja vya ndege 11 na amepongeza juhudi mbalimbali zinazofanywa na
nchi nyingine wanachama wa Afrika Mashariki.
“Nataka
kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge wa Afrika Mashariki kuwa Serikali
ninayoiongoza itaendelea kushirikiana na Bunge hili katika masuala
mbalimbali ya kuiunganisha jumuiya yetu, na ninawaomba nanyi mtekeleze
wajibu wenu wa kuwaunganisha na kuwaelimisha wananchi ili waone umuhimu
wa jumuiya hii” amebainisha Mhe. Rais Magufuli.
Kwa
upande wake Spika wa Bunge la Afrika Mashariki Mhe. Martin Ngoga
amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kulihutubia Bunge hilo na amempongeza kwa
jitihada zake za kujenga nidhamu ya utumishi wa umma, kuzidisha
mapambano dhidi ya rushwa, kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo,
kukuza uwekezaji na biashara ikiwemo ujenzi wa viwanda na kuonesha
uongozi mahiri, na ametoa wito kwa Watanzania kuunga mkono juhudi hizo.
Pamoja
na Wabunge wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, viongozi wengine
waliohudhuria wakati Mhe. Rais Magufuli akihutubia bunge hilo ni Waziri
Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Naibu wa Pili wa Waziri Mkuu wa
Uganda Mhe. Kirunda Kivejinja, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Job Yustino Ndugai, Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi John
Kijazi, Mawaziri, Mabalozi wanaowakilisha nchi mbalimbali hapa nchini,
viongozi wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama na Wabunge wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dodoma
24 Aprili, 2018
0 comments:
Chapisha Maoni