Mbunge
wa Viti Maalumu (Chadema), Cesilia Pareso amesema ukiacha maadui watatu
wa Taifa ambao ni maradhi, umasikini na ujinga ameongezeka adui namba
nne ambaye ni vyama vya siasa vya upinzani.
Akizungumza
jana Alhamisi Aprili 5, 2018 katika mjadala wa bajeti ya Ofisi ya
Waziri Mkuu mwaka 2018/19 bungeni mjini Dodoma, Pareso alisema vyama vya
upinzani ni adui mwingine kwa kuwa kwa sasa vinapigwa vita na Serikali
iliyopo madarakani, ikiwa ni pamoja na kuzuiwa kufanya shughuli za
siasa.
Mbunge
huyo pia amegusia chaguzi ndogo zilizofanyika hivi karibuni, kubainisha
kuwa zilikuwa ni kati ya Chadema na Jeshi la Polisi sambamba na kueleza
jinsi wabunge na madiwani walivyonunuliwa na kuvihama vyama vyao, nchi
kulazimika kufanyika chaguzi nyingine alizodai aimegharimu zaidi ya Sh6
bilioni.
Maelezo
ya Pareso yalipingwa na baadhi ya wabunge na wengine kumuunga mkono
huku Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba akimjibu mbunge
huyo kuwahusisha polisi na chaguzi mbalimbali.
“Utaendeleaje
kupima chama cha siasa kinakua kama hakifanyi mikutano ya hadhara na
kuongeza wanachama, leo mtu anajiunga kesho mtu anatoka,” alisema
Pareso.
“Kama
mnakataza vyama vya siasa visifanye mikutano ya hadhara, hamuwezi kuja
bungeni na kutueleza vyama hivi vimeendelea kufanya vizuri miaka 26
iliyopita.”
Huku
akizungumza kwa upole Pareso alisema, “Miaka ya nyuma waasisi wa nchi
hii waliwaaminisha Watanzania kwamba kuna maadui watatu ambao ni
umaskini, ujinga na maradhi lakini kwa yanayoendelea leo, jambo jingine
limeongezeka kwa Serikali iliyopo madarakani. Adui mwingine ni vyama vya
siasa.”
Alisema
siku za hivi karibuni wabunge na madiwani wa vyama vya siasa, hasa
upinzani wamekuwa wakiripoti polisi na kuwekwa rumande, hata kama
wataachiwa wataendelea kuripoti polisi.
“Mmeongeza
adui mwingine ambaye ni vayama vya siasa vya upinzani. Tumeshuhudia
kwenye changuzi ndogo za marudi, utumiaji mbovu wa fedha za wananchi.
Kama tulitenga fedha za dharura Sh4bilioni endapo utatokea uchaguzi leo
tumetumia Sh6.9bilioni,” alisema.
“Kwanini
tusingefikiria kuhifadhi hizi hela kuliko kurudisha wananchi kufanya
chaguzi tena kwa sababu tu watu wameamua kununua watu warudi upande wa
pili.”
Alisema
chaguzi hizo za marudio zilikumbwa na ukiukwaji wa taratibu za
uchaguzi, “tumeshuhudia uchaguzi kati ya Chadema na Jeshi la Polisi.
Nilishuhudia wakala anatekwa kituoni polisi yupo na hasemi kitu.”
“Ushauri
wangu kwa Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa) kwa sababu inaonekana
mmeongeza adui mwingine ambaye hamtaki kumsikia, ushauri wangu ni kuleta
marekebisho ya katiba hapa bungeni. Tufute vyama vingi ili ulimwengu
na dunia ijue kwamba Serikali haitaki vyama vingi turudi kwenye mfumo
wa chama kimoja. Hiyo ni njia sahihi na mtaendelea kuyafanya
mnayoyafanya kama mnavyotaka.”
Wakati Pareso akiendelea kuchangia, Mwigulu alisimama na kutoa ufafanuzi wa alichokisema mbunge huyo.
“Pamoja
na kuheshimu uhuru wa kuongea na kulinda uhuru wa mbunge kutoa maoni
yake, nilitaka kuwashauri wabunge tunapoongelea taasisi ambazo zipo
kikatiba na kufanya kazi kwa ajili ya wananchi tuheshimu kazi
zinazofanywa,” alisema Mwigulu.
“Hakuna
uchaguzi kwa uzoefu wangu ambao utafanyika bila usalama kuimarishwa.
Uhalifu wowote unaofanyika ndani ya nchi, iwe wakati wa uchaguzi au
wakati ambao si wa uchaguzi, unahitaji kuwahakikishia wananchi usalama
kama kawaida.”
Mwigulu
alisema uzoefu umeonesha kuwa muongeaji (Pareso) chama chake
kinaposhiriki katika uchaguzi kunakuwa na matukio makubwa ya uhalifu.
“Kuna
uchaguzi mmoja chama chako (Chadema) hakikushiriki hakukuwapo na
matukio ya aina yoyote ya utekaji wala maumivu ya wananchi. Sisi kama
Jeshi la Polisi tupo kwa ajili ya kuwahakikishia wananchi usalama na
hatuwezi kuacha wananchi wakakatana mapanga,” alisema.
Baada
ya maelezo hayo Pareso aliendelea kuchangia, “Naomba kumwambia Mwigulu
kwa sababu unaingia katika baraza la mawaziri, pokea ushauri wangu na
umueleze Rais Magufuli tufute vyama vya upinzani nchini.”
0 comments:
Chapisha Maoni