Na: Lilian Lundo – MAELEZO, Dodoma
Waziri
wa Mambo ya Ndani ya Nchi Dkt. Mwigulu Nchemba amelitaka Jeshi la
Polisi kuwaweka ndani madereva wanaosababisha ajali kutokana na mwendo
kasi na baadaye kupelekwa Mahakamani.
Dkt.
Mwigulu ametoa agizo hilo jana Bungeni Mjini Dodoma alipokuwa akijibu
muongozo wa Mbunge wa Ulanga Morogoro Mhe. Goodluck Mlinga, juu ya
chanzo cha ajali ya basi la City Boy kutoka Karagwe Mkoani Bukoba
kuelekea Dar es Salaam ambalo liligongana uso kwa uso na lori aina ya
Fuso lililokuwa linatoka Singida kuelekea Igunga usiku wa Aprili 04
mwaka huu na kusababisha vifo vya watu 12.
“Hatuwezi
kuacha watu wanapotea kwa ajili ya uzembe wa mtu mmoja na kuleta hasara
na vilio vikubwa kwa Watanzania,” alisema Dkt. Mwigulu.
Amesema,
ajali nyingi zinazotokea hapa nchini zinasabishwa na mwendokasi na sio
tatizo la miundombinu ambapo katika ajali zilizoripotiwa ajali 1500
zilisababishwa na mwendo kasi na ajali 89 zimetokana na miundombinu.
Aidha
Dkt. Mwigulu amesema, Tanzania ni moja ya nchi zenye barabara bora
hivyo ajali nyingi zinazotokea husababishwa na uzembe wa madereva pamoja
na mwendokasi.
Wakati
huohuo bungeni hapo, Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce
Ndalichako amesema Serikali imeweka utaratibu mashuleni wa kuwawezesha
watoto wa kike kuripoti matukio ya udhalilishaji na pia imeanzisha
klabu mbalimbali za kuwajenge uwezo na ujasiri wa kuweza kuripoti
matukio ya udhalilishaji.
Hata
hivyo Prof. Ndalichako amewataka watoto kutokuwa na uwoga wowote kwa
sababu Serikali yao inawalinda, hivyo pale wanapofanyiwa vitendo kinyume
na matakwa ya Serikali watoe taarifa ili Serikali ichukue hatua stahiki
kwa wale wote wanao wadhalilisha na kusababisha watoto wasisome kwa
amani.
0 comments:
Chapisha Maoni