Mdhibiti
na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Prof. Mussa Assad,
ameishauri serikali kufuatilia kwa makini kupaa kwa deni la matibabu
ughaibuni.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana baada ya kuwasilisha bungeni mjini hapa
ripoti yake ya ukaguzi ya mwaka 2016/17, Prof Assad alisema ukaguzi wake
kuhusu gharama za matibabu ughaibuni ulibaini ongezeko kubwa la deni
kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
katika hospitali za India.
Alisema
deni hilo limepanda kutoka kiasi cha Sh. bilioni 28.6 kilichoripotiwa
Juni 30, 2017 hadi Sh. bilioni Sh. 45.73 kufikia Desemba 31, 2017 licha
ya serikali kuweka masharti kwa wananchi kwenda kutibiwa kwenye
hospitali za nje ya nchi.
“Ongezeko
hili ni asilimia 60.71 kwa kipindi kifupi, ni jambo linalohitaji
serikali kulifuatilia kwa makini ili kupunguza mzigo wamadeni na
kuhakikisha kuwa hospitali husika zinalipwa kwa wakati,” alisema.
Kuhusu
Deni la Taifa, Prof. Assad alisema limeongezeka kwa Sh. trilioni 5.04
katika kipindi cha mwaka mmoja kuanzia Juni 2016 hadi Juni 2017.
Alibainisha
kuwa hadi kufikia Juni 30, 2017, deni hilo lilikuwa Sh. trilioni 46.08
likipanda kutoka Sh. trilioni 41.03 lilivyokuwa Juni2016, ikiwa ni
ongezeko la Sh. trilioni 5.04 (asilimia 12).
Alisema kuwa kati yake, deni la ndani ni Sh. trilioni 13.33 na deni la nje ni Sh. trilioni 32.75.
Prof.
Assad alisema kiasi cha Sh. trilioni 4.58 hakikujumuishwa katika Deni
la Taifa kutokana na kutojumuishwa kwa madeni ya mifuko ya pensheni
pamoja na dhamana ambazo masharti yake yalikiukwa.
CAG
Assad alibainisha vigezo vitatu vinavyotumika kupima uhimilivu wa Deni
la Taifa akibainisha kuwa uwezo wa nchi kulipa riba ya deni ulikuwa
umefikia karibu mwisho, lakini mwaka huu wametumia kigezo cha GDP
kulingana na deni hilo.
”Kwa
kutizama kigezo hicho, tumesema ni himilivu, lakini kama nilivyosema
siyo busara kutizama kipengele hicho na kusema tunaweza kukopa kwa
sababu tulishawahi kukopa tukapunguziwa mkopo,” alisema.
”Kwa
hiyo, mimi rai yangu ni lazima tuwe waangalifu katika ukopaji wetu.
Deni la Taifa linapimwa kwa namna nyingi, na zipo namna tatu kubwa; ya
kwanza ni ile ya kuangalia deni kulinganisha na Pato la Taifa, lakini
pia ujue kwamba unachotakiwa kufanya ni kuangalia malipo ya mbele
ulinganishe na thamani ya fedha ya sasa.
”IMF
na Benki ya Dunia (WB) kazi yao ni hiyo kuangalia data (takwimu) za
kila nchi. Njia ya pili ni kuangalia mapato ya nchi dhidi ya Deni la
Taifa. Kwa mfano, tunakusanya kiasi gani cha kodi? Hili ni eneo ambalo
ni ‘sensitive’ zaidi, ile ya mwanzo ni kiunzi cha chini sana ndo maana
unaweza kukuta nchi ina asilimia 200 kwa sababu ni kiunzi cha chini
sana.
”Njia
ya tatu ni kuangalia Deni la Taifa dhidi ya ‘export’ kwa sababu sehemu
kubwa ya Deni la Taifa utailipa kwa fedha za nje.”Alisema mwaka huu kwa
kulinganisha Deni la Taifa na GDP, deni hilo linamilika, lakini lazima
nchi ambayo iliwahi kupewa nafuu ya mkopo, isikimbilie kukopakopa.
”Hatuwezi
kusema tutakopa tutakopa, tutakopa kwa tahadhari kubwa kwa sababu
hatutaki kurudi miaka 20 iliyopita sehemu ambayo tunataka tupewe msamaha
wa madeni,” alisema.


0 comments:
Chapisha Maoni