UONGOZI
wa Jeshi la China umeahidi kuisaidia na kuiunga mkono Urusi kijeshi
kukabiliana na mataifa ya Magharibi dhidi ya mzozo wa kidiplomasia,
vikwazo vya kiuchumi na mazoezi ya kijeshi.
Ahadi
hiyo imetolewa Waziri wa Ulinzi wa China, Wei Feng ambaye yuko Urusi
kuhudhuria mkutano wa saba wa kimataifa wa usalama wa Moscow akiwa
ameambata na ujumbe wa maofisa wa ngazi za juu wa jeshi.
Feng alisisitiza kwamba ziara yake imeratibiwa moja kwa moja na Rais wa China, Xi Jinping.
Alisema
alikwenda Moscow akiwa na ujumbe maalumu kutoka kwa Jinping katika
kipindi hiki ambacho mataifa yote mawili yanaboresha majeshi yao na
ushawishi wao duniani licha ya wasiwasi wa Marekani.
“Naitembelea
Urusi kama waziri mpya wa ulinzi wa China kuionyesha dunia maendeleo ya
hali ya juu ya uhusiano wetu na dhamira imara ya majeshi yetu
kuimarisha ushirikiano wa kimkakati,” alisema Wei wakati wa mkutano wake
na Waziri wa Ulinzi wa Urusi, Sergey Shoigu.
“Pili,
kuisaidia Urusi kuendesha mkutano wa kimataifa wa usalama wa Moscow ili
kuwaonyesha Wamarekani uhusiano wa karibu wa majeshi ya China na Urusi
hasa katika hali ya sasa.
“Tumekuja kuwaunga mkono katika harakati zenu na hali inayowakabili,” aliongeza.
“Upende
wa China uko tayari kuzungumza na Urusi kuhusu wasiwasi na misimamo
yetu ambavyo vinawiana dhidi ya matatizo ya kimataifa katika majukwaa ya
kimataifa pia,” alisema.
Hali
hiyo inakuja huku mataifa hayo mawili yakiingia katika mzozo na
Marekani katika maeneo tofauti kuanzia kijeshi hadi kiuchumi.
Rais
Vladimir Putin wa Urusi na Jinping wa China wanaongoza kile
kinachohesabiwa kuwa majeshi yenye nguvu yanayoshika namba mbili na tatu
duniani nyuma ya Marekani.
Wakati
Marekani imeendelea kuongoza kwa kipindi kirefu ikiwaacha kwa mbali
washindani wake linapokuja suala la kijeshi, Moscow na Beijing zinakuja
juu haraka zikilenga kuondoa pengo hilo na kudhibiti ushawishi wa
Marekani katika siasa za dunia.
0 comments:
Chapisha Maoni