SERIKALI
imesema haijazuia vyombo vya habari kukosoa utekelezaji wa sera,
mikakati na programu zake na badala yake imewataka kuzingatia miiko na
maadili ya taaluma hiyo yaliyoanishwa na sheria za kimataifa.
Hayo
yamesemwa jana Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Idara ya Habari
(MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi wakati wa
uzinduzi wa Awamu ya 25 ya utafiti wa sauti ya wananchi iliyotolewa na
taasisi ya Twaweza.
Dkt.
Abbasi alisema kumekuwepo na mkanganyiko mkubwa kuhusu dhana ya uhuru
wa habari, hatua inayosababisha baadhi ya vyombo vya habari kuandika na
kutangaza taarifa mbalimbali ambazo zimekuwa zikikiuka misingi ya sheria
za nchi.
“Wapo
baadhi ya watu wamekuwa wakifikiri dhana ya uhuru ni kusema chochote na
kutumia lugha ya kejeli, hivyo ripoti hii ya utafiti tumeweza kuwa na
wataalamu mbalimbali waliokuwa wakitoa mada na kujadili kwa kina misingi
na miiko ya uhuru wa habari” alisema Dkt. Abbasi.
Alisema
kuwa dhana ya uhuru wa habari ipo katika sheria mbalimbali za kimataifa
iliyoanishwa katika misingi ya haki na wajibu, na hivyo ni wajibu wa
wadau mbalimbali kuwawezesha wananchi na vyombo vya habari nchini kuweza
kuelewa dhana hiyo.
Aliongeza
kuwa Serikali imeendelea kuongeza wigo mpana wa uanzishaji wa vyombo
vya habari nchini ikiwemo kutoa idadi kubwa ya leseni za uanzishaji wa
vituo vya redio hususani katika maeneo ya vijijini, hatua inayolenga
kuwawezesha wananchi kuweza kupata taarifa mbalimbali za umma.
Kuhusu
taarifa ya utafiti huo, Dkt. Abbasi alisema Serikali itatumia taarifa
ya ripoti ya utafiti huo kupata mrejesho na kuainisha maeneo yote ili
kuchambua hoja na kuweza kuangalia maeneo yenye changamoto ili kuweza
kuboresha mfumo wa utoaji na upatikanaji wa taarifa za Serikali kwa
wananchi.
Kwa
mujibu wa Dkt. Abbasi alisema Serikali tayari imetoa maelekezo kwa
Maafisa Habari na Mawasiliano wa Taasisi zote za umma nchini kuweka
utaratibu wa kutoa taarifa zake kwa umma kwa kuwa suala la utoaji wa
taarifa si utashi na badala yake ni utekelezaji wa matakwa ya sheria.
Kwa
upande wake, Mkurugenzi wa Taasisi ya Twaweza, Aidan Eyakuze alisema
katika utafiti huo uliohusisha jumla ya watu 1500, ulionyesha kuwa
wananchi wana imani na taarifa na imani zinazotolewa na Viongozi Wakuu
wa Serikali ikiwemo Rais ikifuatiwa na Waziri Mkuu.
0 comments:
Chapisha Maoni