Baada
ya kuachiwa huru siku ya Jumatano na kukamatwa tena, jana aliyekuwa
Mwanasheria Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Baptister Bitaho
(54) amehukumiwa kulipa faini ya Sh milioni 13.9 au kifungo jela miaka
mitano baada ya kusomewa upya mashtaka na kukiri.
Bitaho
alifikishwa tena katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jana asubuhi
na kusomewa mashitaka nane likiwemo la kufanya kazi nchini bila kibali
na kutoa taarifa za uongo.
Bitaho
ambaye ni Raia wa Burundi, alifutiwa mashtaka yake, na baadae
kukamatwa, alisomewa hukumu hiyo, na Hakimu Mkazi Mkuu, Victoria
Nongwa.
Akisoma
hukumu hiyo Nongwa alisema kuwa mahakama imesikiliza maombi ya pande
zote mbili na kwamba katika kosa la kwanza hadi la saba mshitakiwa
atatakiwa kulipa faini ya Sh laki tano au kifungo jela kuanzia miaka
miwili hadi mitatu na kwamba kosa la nane mshitakiwa atatakiwa kulipa
faini ya Sh milioni 10 au kifungo jela miaka mitano.
Alisema,
kwa taratibu zilizopo, baada ya mshitakiwa kukutwa na hatia anatakiwa
kupelekwa Uhamiaji na kurudishwa nchini kwao ili aombe uraia wa Tanzania
upya.
Kabla
hukumu hiyo kusomwa, Wakili wa utetezi, Aloyce Komba alidai kuwa
mshitakiwa hakuwahi kuvunja sheria ya kijinai kwani alikuwa mwaminifu
na hakuwahi kutoa siri ya nchi licha ya ukimbizi wake.
Komba
pia aliongeza kuwa, tangu mteja wake apate kashfa hiyo, ameathirika
kiuchumi kwa kuwa alitakiwa kustaafu miaka sita ijayo lakini sasa
anakosa mapato yake.
‘’Naomba
mahakama isitoe adhabu kubwa kwa mteja wangu kwani pamoja na ukimbizi
wake, kutokana na vita za mara kwa mara zinazotokea nchini Burundi,
mshitakiwa ameanzisha kituo cha kulelea watoto yatima wa Tanzania na
Burundi hivyo amekuwa na msaada,’’alidai Komba.
Akimsomea
maelezo ya awali (PH), baada ya kukiri mashtaka yake, Mwendesha
Mashitaka wa Uhamiaji, Method Kagoma alidai wazazi wa Bitaho waliingia
nchini mwaka 1958 na kisha kurudi tena mwaka 1972 huku yeye Bitaho akiwa
mtoto mdogo.
Aliidai
baada ya kukua, mshitakiwa huyo alijiunga na elimu ya msingi, sekondari
na vyuo hapa nchini na kwamba mwaka 2001 aliajiriwa na TBS kama
mwanasheria.
Katika
mashitaka yake inadaiwa Mei 19, mwaka huu maeneo ya Ofisi ya Uhamiaji
iliyopo Kinondoni jijini Dar es Salaam, akiwa mkimbizi na Raia wa
Burundi, alitoa taarifa za uongo kwa ofisa wa uhamiaji.
Alidaiwa
kuwa alijitambulisha kuwa ni raia wa Tanzania na kuonesha Kitambulisho
cha Taifa chenye jina lake ambacho alikipata kinyume na sheria huku
akijua kwamba anajiongezea kosa.
Kagoma
alidai, Oktoba 19, 2013 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius
Nyerere wilayani Ilala Dar es Salaam, akiwa mkimbizi na Raia wa Burundi,
alishindwa kutimiza masharti yaliyotolewa Septemba 11, 2013 na Kamishna
Mkuu wa Uhamiaji ambapo alishindwa kurejesha hati ya kusafiria
aliyoipata isivyohalali.
Imeendelea
kudaiwa kuwa, Juni 22, 2011 katika Ofisi za Uhamiaji za Mkoa, alitoa
taarifa za uongo katika fomu ya kuombea hati ya kusafiria CT5 (Ai) yenye
namba 05381440 kwa lengo la kupata hati hiyo.
Aidha
mshtakiwa Bitaho anadaiwa kutoa taarifa za uongo kwa kutoa kiapo
kuonesha kuwa baba yake ni raia wa Tanzania kitu ambacho sio kweli na
kwamba alitoa barua kutoka Ofisi ya Kata ya Yombo Vituka
iliyomtambulisha kuwa ni Mtanzania kwa lengo la kupata hati ya
kusafiria.
Mshitakiwa
Bitaho alitoa pia barua ya kuajiriwa aliyoambatanisha na fomu ya maombi
ya hati ya kusafiria kuonesha ni Mtanzania kitu ambacho alijua si
kweli.
Aidha
anadaiwa kujipatia kadi ya kupigia kura kinyume na sheria na kwamba Mei
19 na pia amejihusisha na kazi kama Mwanasheria Mkuu wa TBS bila kuwa
na kibali.
0 comments:
Chapisha Maoni