Kutokana
na Chama cha Wananchi (CUF) kufungua ofisi mpya za chama hicho katika
eneo la Mtaa wa Idrisa Kata ya Mzimuni, Magomeni wilaya ya Kinondoni
jijini Dar es Salaam, Msajili wa Vyama vya Siasa amesema anaamini chama
hicho kinafanya mambo yake kwa kuzingatia sheria.
Jana
Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, alisema hajapata
taarifa yoyote ya chama hicho, kufungua ofisi mpya zaidi ya kuona katika
vyombo vya habari.
“Ukiondoa
taarifa za kwenye media sijapata taarifa yoyote kutoka CUF labda wawe
wameleta leo (jana), lakini naamini chochote wanachofanya wanaelewa
taratibu wataleta taarifa, “ alisema Jaji Mutungi.
Jaji
Mutungi alisema sheria inawataka wanapofungua ofisi watoe taarifa ndani
ya siku 14, ambazo hazijaisha hivyo anaamini wanajua hilo.
Upande
wa Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad wamefungua ofisi hizo, baada
ya tukio la kuvamiwa katika Ofisi Kuu za Buguruni na kundi la Profesa
Ibrahim Lipumba.
Jaji
Mutungi alisema atakapopokea taarifa rasmi ataangalia kama taratibu
zilifuatwa kwani ufunguaji wa ofisi mpya una taratibu zake.
“Nikiletewa taarifa ndio nitajua kama walifata taratibu au la, ufunguaji wa ofisi una taratibu zake najua wanazijua pia, “ alisema Jaji Mutungi.
Alisema
taarifa hiyo ataipata kutoka kwa mwenyekiti au msemaji wa chama, ambaye
ni katibu mkuu ambao wanatambuliwa na ofisi ya msajili wa vyama vya
siasa.
Akizindua ofisi hiyo Juni 4 mwaka huu, Maalim Seif alisema ofisi hiyo imetolewa na wabunge 40 wa CUF.
Alisema uamuzi wa wabunge hao kumpatia ofisi ya kufanyia kazi hapo ni kitendo cha kiungwana na kiungwe mkono na wanachama wote.
Alisema
kwa miezi 10 sasa, wamekuwa wakishindwa kufanya kazi kwa upande wa
Tanzania Bara, jambo ambalo limewaathiri hivyo kupatiwa ofisi
kutamsaidia kutimiza majukumu bila hofu yoyote.
Katibu huyo alisema ana imani na mahakama kuwa itawapatia haki stahiki hivyo kuwataka wanachama kuendelea kuwa na subira.
0 comments:
Chapisha Maoni