Mkuu
wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella amewazuia wakuu wa wilaya na
wakurugenzi wa halmashauri zote mkoani humo kutoka nje ya vituo vyao vya
kazi hadi watakapofikia lengo la kukusanya asilimia mia ya mapato ya
ndani kabla au ifikapo Juni 30, mwaka huu.
Akihutubia
mkutano wa mwaka wa Jumuiya ya Serikali za Mitaa (Alat), Mkoa wa Mwanza
mjini Nansio, Ukerewe leo , Mongella ameonya kuwa wakuu wa wilaya na
wakurugenzi ambao halmashauri zao zitashindwa kufikia malengo watakuwa
wamepoteza sifa za kuendelea kushika nyadhifa zao.
"Hata
wenyeviti na mameya ambao halmashauri zao zitakusanya chini ya asilimia
mia watasalia kwenye nafasi zao kwa sababu tu wamechaguliwa kwa kura,
lakini watakuwa wamedhihirisha udhaifu wao katika usimamizi," amesema Mongella
Amesema
hadi kufikia robo tatu ya mwaka wa fedha 2016/17, halmashauri zote nane
za Mkoa wa Mwanza zilikusanya mapato kwa asilimia 51 pekee.
"Asilimia
49 iliyosalia lazima zikusanywe ifikapo Juni 30, mwaka huu. Namna
mtakavyofanya mimi sijui. Lakini tusije tukaelewana vibaya muda huo
ukifika bila makusanyo kufikia asilimia mia moja."
Mkoa wa Mwanza una wilaya saba za Ilemela, Nyamagana, Ukerewe, Kwimba, Magu, Sengerema na Misungwi zenye halmashauri nane.