WIZARA ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, imesema hakuna uthibitisho wa kuwepo kwa ugonjwa wa Zika nchini.
Ufafanuzi
wa Wizara hiyo umekuja siku moja baada ya Taasisi ya Utafiti wa
Magonjwa ya Binadamu (NIMR), kutoa ripoti ya utafiti uliofanywa na
taasisi hiyo kwa kushirikia na Chuo Kikuu cha Kanisa Katoliki Bugando,
inayoeleza kuwepo wa maambukizi ya virusi vya Zika katika jamii ya
Watanzania.
Waziri
wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu
alitoa ufafanuzi huo kwa waandishi wa habari jana, ambapo alisema
wananchi wanapaswa kuondoa hofu kwa kuwa ugonjwa huo haujaingia nchini.
“Napenda
kuwatoa hofu wananchi kwa sasa haijathibitishwa kuwepo kwa ugonjwa wa
Zika nchini…wao walifanya utafiti nchini wa kuchunguza ubora wa kipimo
cha kupima magonjwa ya Zika na Chikungunya, hawakupima kama zika ipo
nchini au hakuna,” alisema Waziri Ummy.
Alisema wizara yake itaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali, kutafiti ili kubaini kama ugonjwa wa Zika upo nchini au la.
Wizara hiyo pia imeshaanda mkakati wa Zika nchini, unaoelekeza kufuatilia ugonjwa huo.
Mganga
Mkuu wa Serikali, Mohammed Kambi alisema, NIMR walichokifanya ni
kufanya utafiti wa kutathmini ufanisi na ubora wa kipimo, ambacho
kinaweza kuja kutafiti magonjwa ya zika na mengine na kwamba kiutaratibu
hizo ni hatua za awali.
Alisema,
taarifa hiyo ya NIMR itafanyiwa tathmini ya kisanyasi ili wanasayansi
wajiridhishe kama ilifuata taratibu zote na matokeo hayo yanaweza
kuendelezwa mbele zaidi na baadae kuweka mikakati ya kuzidi kuthibisha
uwepo wa ugonjwa huo.
“Tuna
taratibu hizo za upande wa kitaalamu lakini kuna taratibu katika kutoa
tamko, kuhusu uwepo wa ugonjwa kama huu kwasababu ni aina ya uginjwa
unaotakiwa uripotiwe kimataifa…inabidi taarifa ije rasmi katika wizara,
kuna mganga mkuu na Shirika la Afya tuangalie hizo na tukijidhihirisha
taarifa rasmi inatolewa na mratibu wa magonjwa hayo,” alisema Dk
Mohammed.
Kwa
upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa NIMR, DK Mwele Malecela alisema
taarifa aliyoitoa juzi, ilikuwa ni matokeo ya utafiti wa kubainisha
uwezo wa kipimo hicho katika kuanisha virusi vya Zika, Dengue na
Chikungunya na matokeo ya awali yalionesha uwepo wa virusi vya Zika.
Alisema pamoja na matokeo hayo, hawakuona dalili wala madhara yoyote yanayosababishwa na Zika ikiwemo Kichwa kidogo na mengine.
“Hili
suala ni kwamba lilikuwa ni suala la kuainisha na katika uanishaji huo
tukajikuta tumeona virusi hivyo, lakini hiyo haimanishi kuna
uthibitishio, naomba nisisitize uthibitisho wa ugonjwa unatolewa na
wizara ya afya kwa kufuata uatartibu maalumu uliowekwa,” alisema.
Alisema
kuwa wataendelea kufanya utafiti hasa katika kuangalia magonjwa ya
Zika, Dengue na Chikungunya na kutoa matokeo kwa kile watakachokipata
katika utafiti huo.
Juzi
NIMR ilitoa matokeo ya utafiti uliofanywa na taasisi hiyo pamoja na
Chuo Kikuu cha Katoliki cha Bugando na utafiti kuanisha uwepo wa
maambukizi ya virusi vya zika katika jamii ya Watanzania na kuangalia
adhati ya maambukizi katika kusababisha watoto wanaozaliwa na ulemavu.
Sampuli
za damu kutoka kwa watu 533 zilipimwa. Kati yao, watoto wachanga 80
walizaliwa na ulemavu wa viungo mbalimbali. Kati ya waliopimwa 533, 83
(15.6%) waligundulika kuwa wameambukizwa virusi vya Zika.
Kati
ya wale watoto wachanga 80 waliozaliwa na ulemavu, 43.8% walikuwa
wameambukizwa virusi vya Zika, utafiti unaendelea kujua ukubwa wa tatizo
hili.