Mahakama
Kuu Kanda ya Arusha, imelikubali ombi la Mbunge wa Arusha Mjini
Godbless Lema, la kuongezewa muda wa kuwasilisha Notisi ya nia ya
kukata rufaa ya dhamana yake.
Akitoa
uamuzi wake kuanzia saa 12:26 hadi saa saba mchana, Jaji Dk. Modesta
Opiyo wa Mahakama hiyo, alisema Mahakama hiyo imeruhusu maombi ya
kuwasilisha Notisi ya kuomba kuongezewa muda wa kuwasilisha notisi ya
nia ya kukata rufaa ya dhamana yake.
Jaji
Opiyo amesema hoja za Upande wa serikali zilizowasilishwa na Wakili
Hashim Ngole za kudai waleta maombi hayo walikuwa wazembe na walichelewa
siku nne kuwasilisha Notisi baada ya rufaa yao kuondolewa na Jaji
Fatuma Masengi Desemba 2 hazina mashiko.
Alisema
kuondoa kesi mahakamani haimaanishi kuwanyima fursa ya kupigania nia ya
kukata rufaaa, bali milango inakuwa wazi haijafungwa.
Aidha
amesema siku nne zinazolalamikiwa kuwa walichelewa kutoa maombi hayo,
mahakama inaona hoja hizo hazina mashiko sababu siku mbili kati ya hizo
zilikuwa siku za mapumziko Jumamosi na Jumapili, hivyo walitumia siku
mbili kuandaa nyaraka na kuleta maombi hayo.
Pia alisema katika maombi hayo wametoa pia sababu za nia ya kutaka kukata rufaa na sababu hizo ziko wazi.
“Katika
hili hakuna uvunjifu wowote wa sheria uliofanywa na kutokana na hilo
Mahakama hii inatumia busara zake kuruhusu maombi haya ya kutoa Notisi
ya kuomba kuongezewa muda wa kukata rufaa juu ya dhamana yake Mbunge
huyu,” alisema Jaji Opiyo.
Amesema
Mahakama inatoa siku kumi pekee kuanzia uamuzi huo utolewa mleta maombi
(Lema) kuwasilisha Notisi yake ya kuomba kuongezewa muda wa kukata
rufaa.
Baada ya kutolewa kwa maamuzi hayo, tayari Wakili Sheck Mfinanga ameshakata Notisi Mahakama Kuu Kanda ya Arusha na kupokelewa.
Mfinganga amesema wanasubiri mahakama ili wapangiwe Jaji waendelee na kesi hiyo ya hatma ya dhamana ya Lema.