Hatua hiyo ni miongoni mwa mambo ambayo Kamati Kuu ya CCM iliyoketi jana jijini Dar es Salaam ikiongozwa na mwenyekiti wake, Rais John Magufuli ilijadili ikiwa ni sehemu ya tathmini ya uchaguzi huo.
Tangu uchaguzi huo umalizike ambapo mgombea wa CCM, Rais Magufuli
aliibuka na ushindi wa asilimia 58.46 dhidi ya mpinzani wake wa karibu,
Waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa aliyepata asilimia 39.97, madai ya
kuwapo wasaliti waliomuunga mkono yalitawala na kuwekwa mikakati ya
kuwashughulikia kupitia vikao.
Mbali na kusababisha ushindani mkali
dhidi ya CCM, Lowassa aliyehama chama hicho baada ya kuenguliwa katika
mchakato wa urais na kwenda Chadema, aliviwezesha vyama vinavyounda
Ukawa kupata wabunge 116, idadi kubwa kuwahi kufikiwa tangu mfumo wa
vyama vingi uanzishwe.
Pamoja na Lowassa kuhamia upinzani, mwanasiasa
huyo aliendelea kuungwa mkono ndani ya CCM na mara kadhaa ametoa kauli
zinazoonyesha kuwa bado ana wafuasi ndani ya chama hicho.
Wakati
akikabidhi chama kwa Rais Magufuli, mwenyekiti aliyemaliza muda wake na
Rais mstaafu, Jakaya Kikwete alimkabidhi pamoja na ripoti ya uchaguzi
ikiwa na orodha ya wanaodaiwa kukisaliti chama kutoka maeneo mbalimbali
nchini wakisubiri hatua za vikao vya juu.
Akizungumza na waandishi wa
habari jana, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema
tathmini hiyo inafanyika kwa lengo la kukiimarisha chama kwa chaguzi
zijazo.
“Agenda iliyozungumzwa leo ni tathmini ya uchaguzi wa mwaka
2015. CCM iliagiza ngazi zake za mashina, kata wilaya na mikoa, wafanye
tathmini ya uchaguzi wa mwaka 2015 wa madiwani, wabunge na rais.
“Tathmini hiyo ilikuwa ni pana, imefanyika kwa kipindi cha mwaka mzima.
Mikoa na wilaya zake na kata zao na matawi yake na mashina yake,
wameagizwa wakaleta Kamati Kuu ya chama,” alisema Nape ambaye pia ni
waziri wa habari, utamaduni, michezo na sanaa.
Alisema tathmini hiyo
ilipitiwa na sekretarieti ya chama kabla ya kupelekwa kwenye Kamati Kuu
ambako nako itapelekwa kwenye Halmashauri Kuu kwa maamuzi zaidi.
“Baada
ya kujadiliwa na Kamati Kuu itapelekwa kwenye kikao cha NEC ambacho
ndicho kikao cha maamuzi , kitatoa maelekezo ya mambo ya kufanya na
hatua za kuchukua,” alisema Nape.
“Nisingependa kuzungumzia sana nisije
ku-pre empty NEC, ninachoweza kusema ni kwamba chama kimepokea tathmini,
wanachama wametoa mawazo yao, maoni yao wameleta kwenye vikao, tusubiri
maamuzi ya vikao. Ndiyo siri ya uimara wa CCM,” alisema bila
kuzungumzia ajenda nyingine zilizojadiliwa.
Hatua ya CCM kufanya tathmini hiyo imekuja wakati wakiwapo baadhi ya makada ambao hawakuridhishwa na uamuzi wa Kamati Kuu ya chama hicho kukata jina la Lowassa.
Hatua ya CCM kufanya tathmini hiyo imekuja wakati wakiwapo baadhi ya makada ambao hawakuridhishwa na uamuzi wa Kamati Kuu ya chama hicho kukata jina la Lowassa.
Katika mchakato wa kumpata mgombea urais wa CCM uliofanyika
Julai 2015, baadhi ya wajumbe akiwamo Dk Emmanuel Nchimbi, Sophia Simba
na Adam Kimbisa ambaye ni mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma, walipinga
hadharani hatua ya kukata majina ya wagombea kinyume cha kanuni za chama
hicho, hali iliyoelezwa kuwakera viongozi wakuu wa chama hicho.
Akihutubia mkutano wa kumkabidhi uenyekiti wa CCM Julai 23, 2016 mjini
Dodoma, Mwenyekiti mstaafu Jakaya Kikwete alisema mchakato wa kumpata
mgombea urais wakati huo ulikuwa mtihani mgumu uliotishia kukigawa chama
hicho.
“Mi nadhani katika historia ya CCM hakuna wakati kulikuwa na
tishio la kugawanyika kama mwaka jana.
“Tumeingia kwenye NEC haijapata kutokea ya namna ile. Lakini tukasema
hatutayumba, maadamu sisi viongozi juu tumeshikamana, tutashinda,”
alisema Rais Kikwete.
Lakini akihutubia mkutano huo baada ya kukabidhiwa
uenyekiti Julai mwaka huu, Rais Magufuli aliwataka wanachama
wanaokisaliti chama hicho kutubu au waondoke mara moja.
“Tunataka tukomeshe usaliti
ndani ya chama. Katika uongozi wangu na ninaomba Mungu anisaidie na
mnisaidie tushikamane ndugu zangu, nitahakikisha usaliti unakomeshwa,”
alisema Rais Magufuli na kuongeza:
“Ndani ya chama chetu pamekuwa na
tabia ya baadhi ya wanachama kusaliti chama. Asubuhi anakuwa CCM usiku
yuko Chadema, au yuko chama kingine. Wasaliti wa namna hii hawatakuwa na
nafasi katika uongozi wangu. Kama wapo wenye tabia hiyo, ni vema
wakajirekebisha na kutubu kuanzia leo.
“La sivyo watupishe ikiwezekana
hata leo, waondoke. Ni vema kuishi na mchawi kuliko kukaa na msaliti. Na
hili lazima niliseme na ninalisema kwa dhati. Narudia tena, kama wapo
watubu kuanzia leo.”
Alisema katika uongozi wake anataka wanachama waadilifu wanaofuata Katiba na maadili ya chama chetu, siyo ndumilakuwili.
Alisema katika uongozi wake anataka wanachama waadilifu wanaofuata Katiba na maadili ya chama chetu, siyo ndumilakuwili.
“Hatuhitaji CCM pandikizi na wana CCM masilahi ambao wapo
CCM kwa sababu wanamwabudu mtu fulani kwa masilahi yao binafsi.
Ninahitaji wana CCM ambao siku zote, usiku, mchana, mvua ikinyesha, jua
likichoma, njaa ikiuma, shibe wameshiba, watabaki CCM bila kuyumba.”
Akizungumzia baadhi ya wanachama waliokihama chama hicho wakati wa
uchaguzi na kurejea, Rais Magufuli aliwafananisha na ng’ombe waliokatika
mikia.
“Sisi wachunga ng’ombe, nafahamu hata mzee wetu Kikwete kwa
sababu ana ng’ombe. Ng’ombe akikatika mkia humzuii kuingia zizini, japo
wenzake watajua huyu hana mkia,” alisema Rais Magufuli ambaye pia
alisema yeye hana uvumiliku wa Kikwete, na kuwa kama angekuwa yeye wale
walioimba wana imani na fulani (Lowassa), nusu au robo wangepotea.
Alikuwa anamaanisha wajumbe wa Halmashauri Kuu walioimba wimbo wa
“Tuna imani na Lowassa” mara baada ya Kamati Kuu kukata jina la
mwanasiasa huyo.